POSTA KUSHIRIKIANA NA EQUITY BANK
POSTA KUSHIRIKIANA NA
EQUITY BANK
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo amekutana na kufanya mazungumzo ya kibiashara na Uongozi wa Benki ya Equity Tanzania, Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliofanyika leo tarehe 30 Oktoba, 2021, ulilenga kujadili namna ambavyo taasisi hizi mbili zinaweza kushirikiana katika kutoa huduma za kibenki kwa wananchi kupitia mtandao mpana wa Posta ulionenea nchi nzima.
Aidha, kupitia mkutano huo taasisi hizo zimeweza kuelezea fursa mbalimbali zinazopatikana ili kuboresha na kurahisisha huduma kwa wananchi hasa katika nyanja za Duka Mtandao la Posta, huduma za uwakala na fedha pamoja na huduma za Usafirishaji
Kupitia huduma hizo kutafunguka fursa mbalimbali kwa mwananchi za kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha, urahisi wa malipo kwenye mitandao, kwa upande wa Benki ya Equity wametaka Shirika la Posta litumie fursa hiyo kutoa huduma na Shirika litatoa huduma za Usafirishaji kwa Benki ya Equity ili kila Taasisi inufaike na ushirikiano huo.
Ujumbe kutoka Benki ya Equity uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Esther Kileo Kitoka akiambatana na Viongozi wengine waandamizi wa Benki hiyo.
Kwa upande wa Shirika la Posta Tanzania, mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Shirika.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.
30 Oktoba, 2021.
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo (Kulia) akizungumza wakati wa mkutano na uongozi wa Benki ya Equity. Wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Esther Kileo Kitoka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Esther Kileo Kitoka akizungumza wakati wa mkutano huo.
Mkuu wa Kitengo cha Malipo ya Kidigitali Ralph J. Ligallama akiwasilisha mada wakati wa mkutano huo.
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo (aliyekaa kulia) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Equity Benki pamoja na Baadhi ya wajumbe Menejimenti ya Shirika la Posta nchini. Aliyekaa kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Esther Kileo Kitoka.