📍SHIRIKA LA POSTA LAUNGA MKONO JITIHADA KUKUA KWA UCHUMI WA BULUU ZANZIBAR📍
SHIRIKA LA POSTA TANZANIA LAUNGA MKONO JITIHADA ZA KUKUA KWA UCHUMI WA BULUU ZANZIBAR KWA KUKABIDHI VITENDEA KAZI.
Leo 06/11/2021, Zanzibar
Katika jitihada za kukuza Uchumi wa Buluu Visiwani Zanzibar, Shirika la Posta Tanzania likiongozwa na Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Bwana Macrice Daniel Mbodo limekabidhi vitendea kazi vipya kwa Shirika la Posta (Zanzibar).
Itakumbukwa tarehe 09/10/2021 katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya Posta Duniani Serikali kupitia Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ililikabidhi Shirika la Posta Tanzania vitendea kazi ikiwemo Magari 13 pamoja na Pikipiki 20.
Mgawanyo wa Vitendea kazi hivyo umeenda sambamba kwa kuunga mkono jitihada za kukua kwa Uchumi wa Buluu wa Zanzibar kwa kukabidhi Gari 1 pamoja na Pikipiki 2 zitakazo tumika katika kuimarisha Biashara za Shirika la Posta Zanzibar katika nyanja mbalimbali ikiwemo Usafirishaji na Usambazaji Barua, Vipeto, Vifurushi na Bidhaa mbalimbali za wateja.
Halfa ya makabidhiano hayo yamefanyika katika makao makuu ya Ofisi za Posta Zanzibar ikiwa ni siku ya Maadhimisho ya Mwaka mmoja wa kuwa Madarakani wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Bwana Mbodo amesema kuwa Vitendea kazi hivyo vikatumike katika kuimarisha Biashara za Shirika la Posta Zanzibar,
"Natarajia Vitendea kazi hivi ninavyoenda kuvikabidhi leo hii vitatumika kwa tija ili kuimarisha Biashara za Shirika Zanzibar katika nyanja mbalimbali ikiwemo, Kuimarisha Usafirishaji na kuwahudumia Wananchi katika Usafirishaji wa Barua, Vipeto, Vifurushi". Alisema Mbodo.
Vilevile,Kaimu Postamasta Mkuu, Bwana Mbodo aliendelea kuwasisitiza Viongozi wa Shirika la Posta Zanzibar kuvitunza Vitendea kazi hivyo ili kufikia azma ya kutekeleza Mkakati wa Shirika na Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025,
"Ili kufikia azma ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Shirika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na Vipaumbele vyetu, Nawasisitiza kuvitunza Vitendea kazi hivi na niwaombe vitumike kwa lengo la uzalishaji kama ilivyokusudiwa" Alisema Mbodo
Aidha, Kaimu Postamasta Mkuu alimalizia kwa kusema Shirika la halitamvumilia Mtumishi yeyote atakayetumia Vitendea kazi hivyo kinyume na Malengo,
"Shirika halitamvumilia Mtumishi yeyote atakayetumia vitendea kazi hivi kinyume na Malengo yaliyokusudiwa, Niwaase tena kufanya kazi kwa bidii, weledi na kujituma ili tuweze kukuza mapato ya Shirika letu na Uchumi wa nchi yetu kwa ujumla" Alisema Mbodo
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.
06 Novemba, 2021.
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo (wa pili kushoto) akiwa kwenye hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Shirika la Posta (Zanzibar). Kushoto ni Meneja Mkaazi Zanzibar Bw. Ahmad Mohamed Rashid na kulia ni viongozi waandamizi wa Shirika la Posta, mjini Zanzibar.
Baadhi ya Watendaji wa Shirika la Posta (Zanzibar) wakifuatilia hafla ya makabidhiano ya vitendea kazi kwa Shirika hilo, iliyoongozwa na Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Bw. Macrice Daniel Mbodo, mjini Zanzibar
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo akizungumza wakati wa hafla hiyo.