📍POSTA KUCHANGIA MAENDELEO YA UCHUMI WA BULUU ZANZIBAR📍

POSTA KUCHANGIA MAENDELEO YA UCHUMI WA BULUU ZANZIBAR

 Yaahidi kutangaza utalii kupitia stempu zake

 Duka mtandao lanufaisha wajasiriamali wa Zanzibar

 

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo ameeleza namna ambavyo Shirika hilo limejipanga katika kuhakikisha linakuwa moja ya taasisi za Serikali itakayochangia kukuza maendeleo na uchumi Visiwani Zanzibar.

Ameyasema hayo leo tarehe 23 Novemba, 2021 wakati akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Rahma Kassim Ali, katika ofisi za Wizara hiyo Kisauni, Zanzibar

Bw.Mbodo ameeleza kuwa, Shirika la Posta nchini linatambua mchango wa Wizara hiyo katika kutengeneza mazingira rafiki hususani kwa wananchi wa Zanzibar katika kutumia huduma za Posta nchini, hasa katika matumizi ya Duka Mtandao lililoanzishwa na Shirika la Posta Tanzania.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara yake ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa upande wake imeendelea kuhamasisha wajasiriamali wadogowadogo na wakubwa visiwani humo kujisajili kwenye Duka hilo kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za Zanzibar duniani kote kupitia Duka hilo

“Posta tunajivunia uwepo wa Wizara hii na jitihada kubwa ambazo zimefanywa na Wizara hii katika kutengeneza mazingira rafiki ya Shirika la Posta kuwahudumia wananchi ikiwemo kuwasajili wajasiriamali wa Zanzibar kwenye Duka Mtandao la Posta ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za Zanzibar duniani”. Amesema Mbodo.

Itakumbukwa wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani tarehe 9 Octoba, 2021 Shirika la Posta Tanzania liliandaa shindano kwa mjasiriamali atakayeonekana kuuza bidhaa nyingi zaidi nje ya nchi kupitia Duka Mtandao la Posta, ambapo mshindi alikuwa ni Zanzibar State Trade Cooperation (ZSTC) kutoka Zanzibar na alikabidhiwa zawadi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango, jijini Dododma.

“Takwimu za Mauzo ya Duka mtandao zinaonesha kuwa Zanzibar imeuza bidhaa mbalimbali nje ya nchi hususani viungo na hilo linaonesha kuwa bidhaa kutoka Zanzibar zinahitajika duniani,” Amesema Mbodo.

Katika hatua nyingine, Bw. Mbodo alifafanua kuwa, Shirika la Posta limejipanga kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutangaza vivutio vya Utalii kwa kutumia stampu zinazotengenezwa na Shirika hilo lengo ikiwa ni kukuza sekta ya utaliii Visiwani Zanzibar.

Aidha, Stempu hizo zenye vivutio mbalimbali ikiwemo Majengo ya kihistoria ya Zanzibar, Maraisi waliomaliza muda wao visiwani humo zinaweza kupata fursa ya kuuzwa na kupatikana sehemu zote duniani kupitia wakusanyaji wa stempu hizo zaidi ya 60 walioko zanzibar ikiwa ni sehemu ya kukuza Sekta ya utalii nchini.

 Bw. Mbodo ameongeza kuwa, Shirika la Posta nchini kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Utalii ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar litatambulisha na kutangaza zaidi aina za vivutio vinavyopatikana Zanzibar na kuziweka katika Stampu sambamba na duka Mtandao ili kuvutia watalii wengi  zaidi duniani

Vilevile Shirika la Posta Tanzania limejipanga kuhakikisha linakuwa miongoni mwa taasisi zitakazochangia maendeleo ya ukuaji wa uchumi Visiwani Zanzibar kwa kuendelea kutoa huduma bora na stahiki zenye tija kwa wanachi wa Zanzibar kulingana na mahitaji ya soko.

“Tunaiomba Serikali ya Mapinduzi zanzibar kuendelea kutoa ushirikiano kwa Shirika la Posta ili liweze kuwa miongoni mwa taasisi ambazo zinaweza  kuchangia maendeleo ya uchumi wa buluu Zanzibar”. Amesema Mbodo

Wakati huo huo, Kaimu Postamasta Mkuu ameelezea mashirikiano yaliyopo baina ya Shirika la Posta Tanzania na Taasisi mbalimbali zilizopo visiwani Zanzibar ikiwemo Shirika la Bima Zanzibara (ZIC), Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), lengo ikiwa ni kuhakikisha wananchi wa pande zote mbili za Muungano wanapata huduma stahiki na kwa wakati.

“Shirika la Posta ni Taasisi ya Muungano na tuna ofisi zaidi ya 350 kote nchini, kwa hiyo tunaweza kurahisisha wananchi kufikishiwa huduma kokote walipo nchini”. Amesema Mbodo.

Katika hatua nyingine, Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta alipata nafasi adhimu ya kukabidhi Zawadi ya saa maalumu kwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (Zanzibar) Mhe. Rahma Kassim Ali pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndg. Amour Hamil Bakar zenye Nembo ya Shirika la Posta, picha za stempu zenye vivutio vilivyopo Zanzibar, picha ya magari kuonesha huduma ya usafirishaji, na Duka mtandao la Shirika ikiwa ni sehemu ya huduma za Shirika la Posta zenye lengo la kukuza maendeleo ya uchumi wa buluu Zanzibar. 

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali amelipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa kazi kubwa na maboresho makubwa yanayofanywa na Shirika hilo katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora Zanzibar na nchini kote.

“Niwapongeze kwa shughuli ambazo mnazifanya ikiwemo kuitangaza Zanzibar kiutalii, hiyo itapelekea kuvutia watalii wengi zaidi hatimaye kukua kwa uchumi Zanzibar. Alisema Mhe. Rahma”.

Aidha, Mhe Waziri amelitaka Shirika la Posta nchini kuendelea kuwekeza katika kujitangaza zaidi hasa kwa upande wa Zanzibar ili wananchi waendelee kuvutiwa zaidi na uboreshwaji wa huduma mbalimnali zilizofanywa na Shirika la Posta nchini pamoja na kutumia fursa mbalimbali za Shirika hilo

“Hili ni Shirika  la wananchi wanapaswa kulijua kwa sababau na wao watatumia fursa hizo katika shughuli zao mbalimbali.”. Alisema Mhe. Rahma

Mhe Waziri ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Shirika la Posta nchini ili kuhakikisha wananchi wa pande zote za Muungano wanapata huduma bora na zenye tija kwa manufaa ya Taifa.

Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Meneja Mkaazi Zanzibar akiambatana na viongozi waandamizi wa Shirika la Posta Tanzania

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano;

Shirika la Posta Tanzania.

23 Novemba, 2021.

 

CB9EBEF5 B6BF 4FFA A7EF 8A0FE451110F

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo akiwa ofisini kwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali kabla ya kuanza kwa mkutano

A6E187D6 50D7 4B6C 96C0 C5F5F2E7085E

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali (kulia) akizungumza wakati wa mkutano huo

C8160467 505F 43A8 929B AE8D3BC46116

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Ndg. Amour Hamil Bakar akizungumza wakati wa mkutano huo

417C43A4 BFF8 49A9 AF86 2B6C84BBFAD8

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo akizungumza wakati wa mkutano huo

3B1AAAE0 5961 40C1 AFF8 1EB5539517BF

Viongozi waandamizi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakifuatilia mkutano huo

DBF1F20F 8DB0 4531 877D 89C3CF0B1F1D

Viongozi waandamizi wa Shirika la Posta Tanzania wakifuatilia mkutano huo

F76BB4E4 31A7 4BB7 AC7D 1CE047E93973

BE061B0F 3E77 44A4 93F2 7EEF1CB774AE

01E5B970 07A0 412D 8A14 2E00857897D2

E859C6E4 A953 4F3B 9BC2 9BA706ED1020

 

 

Tanzania Census 2022

X

Tanzania Posts Corporation

You have no authorized to right click contents of TPC, All rights reserved!