Loading . . .

News Single

News Single

POSTA NA ZDCEA ZAIMARISHA USHIRIKIANO KUTOKOMEZA DAWA ZA KULEVYA

Blog Single

Shirika la Posta Tanzania limeingia makubaliano ya kimkataba na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA), kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia nyaraka, vipeto, vifurushi na mizigo ndani na nje ya Zanzibar.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) iliyofanyika Migombani, Zanzibar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Anna Athanas Paul, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuziba mianya inayoweza kutumiwa na wahalifu kusafirisha dawa za kulevya kupitia huduma za posta.

Amesisitiza kuwa makubaliano hayo yanapaswa kutekelezwa kwa vitendo kupitia kubadilishana taarifa za kiintelijensia na kuimarisha ukaguzi wa mizigo na vifurushi.

Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo, amesema ushirikiano huo utaimarisha uwezo wa kitaaluma na kiteknolojia kwa kubaini na kuchukua hatua dhidi ya vifurushi vinavyotumika kusafirisha dawa za kulevya.

Amesema Shirika la Posta litaendelea kuhakikisha mtandao wake unatoa huduma salama na hauwi njia ya kupitisha bidhaa haramu, huku likiahidi kutoa ushirikiano wote unaohitajika ili makubaliano hayo yatekelezwe kikamilifu.

Naye Kamishna Mkuu wa ZDCEA, Kanali Burhan Zuberi Nassoro, amesema mabadiliko ya mbinu za usafirishaji wa dawa za kulevya, ikiwemo matumizi ya mifumo ya usafirishaji wa mizigo, yameifanya taasisi hiyo kuona umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na Shirika la Posta Tanzania.

Amesema makubaliano hayo yataongeza ufanisi katika kubaini na kudhibiti dawa za kulevya, ikiwemo dawa za viwandani na kemikali bashirifu, kupitia matumizi ya teknolojia, mifumo ya ukaguzi na mafunzo kwa watumishi na wafanyakazi.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuimarisha usalama wa huduma za posta na kuongeza nguvu katika juhudi za pamoja za kuzuia usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, kulinda afya za wananchi na kuokoa kizazi cha sasa na kijacho.

Imetolewa na;
Kitengo Cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.