POSTA YAENDELEA KUIUNGANISHA TANZANIA KWA USAFIRISHAJI, YASHIRIKI UZINDUZI WA XERIN MARKET
Shirika la Posta Tanzania (TPC) limeendelea kuimarisha nafasi yake kama mdau muhimu na bingwa wa usafirishaji na usambazaji wa bidhaa nchini, baada ya kushiriki katika uzinduzi rasmi wa jukwaa la biashara, Xerin Market, hatua inayolenga kuunganisha biashara na huduma za usafirishaji ili kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Uzinduzi huo uliofanyika, Novemba 11, 2026, Kariakoo Jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw. Ephraim Mafuru, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, huku Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Posta Bw. Ferdinand Kabyemela akimwakilisha Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Kabyemela amesema, mafanikio ya kibiashara hayaishii katika kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi kupitia teknolojia pekee, bali yanategemea pia uwepo wa mfumo madhubuti wa usafirishaji na usambazaji wa bidhaa unaotolewa na Shirika la Posta.
Uzinduzi wa Xerin Market unaongeza fursa ya kuunganisha wafanyabiashara wa Kariakoo na maeneo mengine nchini na masoko mapana zaidi, huku ushirikiano na Posta ukiweka msingi wa kuimarisha huduma za usafirishaji na usambazaji wa bidhaa kwa wateja.

Kupitia ushiriki wake katika jukwaa hilo, Shirika la Posta Tanzania linaendelea kuthibitisha umuhimu wake katika sekta ya usafirishaji kwa kutumia miundombinu yake kuunganisha watu, biashara na fursa, huku likiendelea kuweka mbele utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Imetolewa na;
Kitengo Cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.