BODI YA POSTA TANZANIA YAKUTANA NA UONGOZI WA PAPU KUJADILI MAENDELEO YA SEKTA YA POSTA
Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) imefanya ziara ya kikazi katika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), PAPU Tower, jijini Arusha, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kutambua fursa za maendeleo ya sekta ya posta barani Afrika.
Msafara huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Salim Milanzi, akiambatana na Makamu Mwenyekiti, Bw. Toyi Ruvumbagu na wajumbe wa bodi, Postamasta Mkuu, Bw. Macrice Mbodo na Menejimenti ya Shirika. Walipokelewa na Katibu Mkuu wa PAPU, Dkt. Sifundo Chief Moyo, pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Bi. Jessica Hope Ssengooba.
Mazungumzo yalijikita katika maeneo ya ushirikiano ikiwemo mageuzi ya kidijitali, biashara mtandao, huduma za kifedha na ujenzi wa uwezo katika sekta ya posta.
Mwenyekiti wa Bodi alisisitiza umuhimu wa k]uimarisha mahusiano kati ya TPC na PAPU, huku Katibu Mkuu wa PAPU akiwashukuru viongozi wa Shirika kwa ziara hiyo na kuwakaribisha kuendeleza ushirikiano wa karibu.
Ushirikiano huo unaakisi utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tisa wa Kibiashara (9th SBP) na juhudi za kuimarisha ushindani na ubora wa huduma za posta.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania