Loading . . .

News Single

News Single

POSTA YAENDELEA NA MAGEUZI MAKUBWA YA KIUTENDAJI, YALENGA KUIMARISHA HUDUMA KWA WANANCHI NA KUWA KINARA AFRIKA

Blog Single

Shirika la Posta Tanzania limeedelea kuimarish mageuzi ya kiutendaji yanayolenga kuongeza tija, kuimarisha ushindani wa kibiashara, kupanua wigo wa huduma na kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi, katika dhamira ya kujenga Shirika lenye ufanisi na ushindani wa kimataifa.

Hatua hiyo inatekelezwa kupitia mafunzo maalumu ya siku mbili kwa Mameneja wa Mikoa yanayofanyika Novemba 12 hadi 13, 2026, yakilenga kuimarisha uwezo wa viongozi katika kusimamia matokeo, kuunganisha rasilimali na kuongeza uzalishaji katika maeneo yao ya kazi.

Akifungua mafunzo hayo, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo, amesema mageuzi hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tisa wa Kibiashara wa Shirika wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031, unaolenga kuimarisha utendaji wa Shirika kwa kuzingatia nguzo sita zinazokwenda sambamba na mkakati wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema utekelezaji wa mpango huo unahitaji viongozi wenye uwezo wa kubadilisha mipango kuwa matokeo halisi, kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi na kuhakikisha shughuli zote za Shirika zinaongeza thamani kwa wateja, wananchi na Taifa kwa ujumla.

Katika kuharakisha mageuzi hayo, Postamasta Mkuu ameelekeza Mameneja wa Mikoa kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji (Turnaround Strategy) kwa kuimarisha usimamizi wa biashara, kuongeza uzalishaji, kubuni fursa mpya za mapato na kuhakikisha huduma zote za Posta zinawafikia wananchi na kutumika kikamilifu.

Amesisitiza umuhimu wa kuondokana na utegemezi wa shughuli chache za kibiashara kwa kupanua wigo wa vyanzo vya mapato, kutafuta wateja wapya na kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, ameelekeza kuimarishwa kwa mifumo ya usimamizi na upimaji wa utendaji ili kila Meneja wa Mkoa na kiongozi wa ngazi nyingine awe na malengo yanayopimika, utekelezaji unaofuatiliwa na matokeo yanayotathminiwa kwa wakati.

Kwa upande wa rasilimali watu, amesema ubora wa uongozi na uwezo wa watumishi ni msingi wa ukuaji wa Shirika, hivyo mafunzo hayo yanalenga kujenga uongozi unaowajibika, unaotambua fursa, unaosimamia rasilimali na kuweka mahitaji ya wateja katika nafasi ya kwanza.
Mafunzo hayo pia yanatarajiwa kuimarisha matumizi bora ya rasilimali watu, fedha, mali na miundombinu ya Shirika, kuongeza uwezo wa Mikoa katika kupanga na kusimamia biashara pamoja na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ubora, ufanisi na kasi inayokidhi matarajio ya wananchi.

Amesisitiza kuwa Posta ni mali ya wananchi na watumishi wa Shirika ni watumishi wao, hivyo mageuzi yanayoendelezwa yanapaswa kuleta mabadiliko yanayoonekana katika ubora wa huduma, ufanisi wa biashara na namna wananchi wanavyohudumiwa.

Imetolewa na;
Kitengo Cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.