POSTA TANZANIA YAPATA MAFUNZO YA VIWANGO VYA USALAMA AFRIKA
Shirika la Posta Tanzania (TPC) limepata mafunzo ya viwango vya usalama wa posta vya S58 na S59, yaliyoandaliwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) jijini N’Djamena, nchini Chad kwa malengo ya kuimarisha usalama wa huduma za posta.
Mafunzo hayo yalifunguliwa Novemba 10, 2026 na kuhitimishwa tarehe 12 November, huku ukiwakutanisha wawakilishi kutoka takribani nchi 30 za Afrika, kwa lengo la kuimarisha uelewa na uwezo wa kitaalamu katika utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya usalama na udhibiti wa mifumo ya huduma za posta.
Katika mafunzo, Shirika la Posta Tanzania, linawakilishwa na Mkuu wa Kitengo Cha Mambo ya Ndani, Bw. Mathias Kipeta, pamoja na wataalamu na wadau wengine wa sekta ya posta kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Kupitia mafunzo hayo, washiriki wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha ujuzi utakaosaidia taasisi za posta kukidhi matakwa ya kimataifa kuhusu usalama, uthibitishaji na ulinzi wa mifumo ya usafirishaji wa nyaraka na vifurushi.
Aidha, mafunzo hayo yanalenga kuifanya ajenda ya usalama kuwa msingi muhimu wa kujenga imani kwa wateja, kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha mifumo ya posta barani Afrika ili iendane na mahitaji ya sasa ya sekta hiyo.
Ushiriki wa Posta Tanzania katika mafunzo hayo unaakisi umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuimarisha viwango vya usalama na kuboresha huduma za posta kwa kuzingatia matakwa na viwango vinavyotambulika kimataifa.
Imetolewa na;
Kitengo Cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.