Loading . . .

News Single

News Single

POSTA YATOA MAFUNZO YA HUDUMA KWA WATEJA NA MAWASILIANO

Blog Single

Shirika la Posta Tanzania (TPC) limetoa mafunzo ya huduma kwa wateja na mawasiliano kwa Mameneja wa Posta kutoka mikoa mbalimbali nchini, yakilenga kuimarisha uwezo wa watumishi katika kusimamia utoaji wa huduma bora, kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kukuza ushindani wa biashara ya Shirika.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano, Huduma kwa Wateja na Mawasiliano wa Shirika la Posta Tanzania, Bi. Jamila Mbarouk, amewataka mameneja hao kuweka kipaumbele katika utoaji wa huduma bora kwa wateja, akieleza kuwa wateja ni msingi muhimu wa ukuaji na maendeleo endelevu ya Shirika.

Amesisitiza kuwa kuwahudumia wateja kwa weledi, heshima na ufanisi ni nyenzo muhimu katika kujenga uaminifu, kudumisha mahusiano mazuri na kuongeza imani ya wateja kwa Shirika.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo, Bw. Wilson Vicent Nkutigwa, amesisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia misingi ya uwajibikaji, weledi na ubora wa huduma, akibainisha kuwa utekelezaji wa misingi hiyo utasaidia kuvutia na kudumisha wateja, kuimarisha ushindani wa kibiashara na kuchochea ukuaji wa Shirika.

Aidha, ameeleza kuwa kuridhika kwa wateja, uwasilishaji wa mizigo kwa wakati na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wateja kwa haraka na kwa ufanisi ni miongoni mwa viashiria muhimu vya ubora wa huduma, vinavyopaswa kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Kupitia mafunzo hayo, Shirika la Posta Tanzania linaendelea kuimarisha uwekezaji katika rasilimali watu kwa kuwajengea watumishi uwezo na maarifa yanayohitajika ili kuboresha uzoefu wa wateja, kuimarisha imani ya umma na kuongeza ushindani wa Shirika katika soko la huduma za posta na usafirishaji.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.