MKUBWA AMERUDI KIBABE! POSTA YAIMARISHA HUDUMA ZA EMS NCHI NZIMA NA DUNIANI KOTE
Huduma ya Usafirishaji wa Haraka (Express Mail Service – EMS) ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) inarejea kwa nguvu mpya kupitia kampeni ya “Mkubwa Amerudi Kibabe”, inayolenga kuwakumbusha wananchi, wafanyabiashara na taasisi kuhusu uwezo wa EMS katika kufikisha nyaraka na mizigo ndani na nje ya nchi.
Kampeni hiyo imezinduliwa na kuanza kutekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa na matumizi ya EMS kwa kuwaonesha wateja fursa zinazopatikana kupitia mtandao wake mpana wa usafirishaji, unaowaunganisha na maeneo mbalimbali nchini na duniani kote.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Ferdinand Kabyemela, alisema “Mkubwa Amerudi Kibabe” inaakisi nguvu mpya, uzoefu na dhamira ya Shirika ya kuendelea kuwapa wateja huduma bora, za uhakika na zinazokidhi mahitaji yao. Alisisitiza kuwa EMS imerudi kibabe nchini kote na duniani kupitia mtandao wake wa kimataifa.
Alieleza kuwa neno “Mkubwa” linaakisi uzoefu na mtandao mpana wa EMS, huku “Kibabe” likionesha nguvu mpya na dhamira ya kuwahudumia wateja kwa ufanisi zaidi.
Kampeni hiyo inaongozwa na kauli mbiu “Tuma Mzigo Popote Duniani, Tukufikishie Leo Leo,” ikiwahamasisha wananchi kutumia EMS kama suluhisho la usafirishaji wa nyaraka na mizigo kwa urahisi.
Kampeni itaendelea katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha pamoja na Zanzibar, ambapo wataalamu wa Posta watakutana na wananchi ana kwa ana kutoa elimu kuhusu huduma za EMS na kusikiliza maoni yao kwa ajili ya kuboresha huduma.
Kwa upande wake, Bw. Vincent Njau wa Kiredio aliwahimiza wanachuo na wadau mbalimbali, wakiwemo Watanzania wanaoishi nje ya nchi, kutumia EMS kusafirisha nyaraka na bidhaa zao kama dagaa. Alisisitiza urahisi wa huduma hiyo inayomwezesha mteja kufikishiwa mzigo wake mpaka nyumbani.
Shirika la Posta Tanzania linawahimiza wananchi, wafanyabiashara, wanachuo na taasisi mbalimbali kutumia EMS na kunufaika na mtandao wake wa usafirishaji ndani na nje ya nchi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.