Loading . . .

News Single

News Single

POSTA NA DAWA MKONONI ZAINGIA MKATABA KUSAFIRISHA DAWA NA VIFAA TIBA NDANI YA SAA 24

Blog Single

Shirika la Posta Tanzania (TPC) limetia saini makubaliano ya kibiashara na Kampuni ya Dawa Mkononi kwa ajili ya kusafirisha dawa, vifaa tiba, na vifaa vya afya. Ushirikiano huu unalenga kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa mahitaji hayo muhimu katika hospitali, vituo vya afya, na famasi mbalimbali kote nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini  iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shirika la Posta Tanzania, Dar es salaam, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Ferdinand Kabyemela, alibainisha kuwa usafirishaji huo utafanyika kupitia huduma ya haraka ya kusafirisha mizigo na vifurushi (EMS). Alisisitiza kuwa mizigo hiyo itafika katika eneo lolote nchini ndani ya saa 24 pekee.

Aidha, Bw. Kabyemela alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa makampuni na taasisi nyingine nchini kuchangamkia fursa ya kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania. Alieleza kuwa huduma za shirika hilo zimeboreshwa na ni za uhakika, salama, za haraka, na zenye gharama nafuu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Dawa Mkononi, Bw. Joseph Paul, alilipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa ufanisi na ubora wa huduma zake za usafirishaji. Aliwahakikishia wateja na wadau wote wa sekta ya afya kuwa bidhaa zao zitawafikia kwa wakati ndani ya saa 24 kupitia mtandao mpana wa EMS.

Bw. Paul pia alitoa rai kwa wamiliki na wasimamizi wa hospitali za umma na binafsi, vituo vya afya na zahanati, famasi (maduka ya dawa) mbalimbali nchini kujiunga na kutumia huduma za usafirishaji za Shirika la Posta Tanzania ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano,

Shirika la Posta Tanzania.