Habari
POSTA YAWEKA HISTORIA MPYA YA MAGEUZI
Shirika la Posta Tanzania limeweka historia mpya ya kuharakisha mageuzi ya kiutendaji, matumizi ya teknolojia na uboreshaji wa huduma, baada ya kuwakutanisha wafanyakazi wote kutoka maeneo yote nchini katika kikao maalumu kilichofanyika Posta Makao Makuu, jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho ni cha kwanza cha aina yake ambacho kimefanyika kikiwakutanisha wafanyakazi wote nchini katika mkusanyiko mkubwa, ikiwa ni historia mpya katika miaka yote ya Shirika la Posta Tanzania tangu kuasisiwa kwake mwaka 1994.

Dhumuni la kikao hicho ilikuwa kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo mpya wa mageuzi na utendaji wa Shirika, kutathmini utekelezaji wa Mpango Mkakati uliopita na kuweka msingi wa utekelezaji wa Mpango Mkakati mpya wa Tisa wa Kibiashara kwa kipindi cha Miaka mitano ijayo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mgeni rasmi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Tanzania, Balozi Meja Jenerali (Mstaafu), Gaudence Salim Milanzi, alisisitiza umuhimu wa umoja, uwajibikaji na weledi miongoni mwa wafanyakazi katika kufanikisha hatua mpya ya maendeleo ya Shirika.

Aidha, aliipongeza Menejimenti na wafanyakazi kwa mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha maeneo yenye changamoto na kuongeza ufanisi wa utendaji.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Makamu Mwenyeketi wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania Bwana Toyi Ruvumbagu, alisema kwa kipindi kifupi cha Uongozi wa Bodi hii kumekuwa na mageuzi makubwa ya kutia moyo katika Shirika na kusisitiza kuwa mwelekeo ni mzuri, kinachohitajika ni kuendeleza kile kilichoanza kuonekana.

Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo, aliwasilisha mrejesho wa utendaji wa Shirika kwa mwaka wa fedha 2025/2026,huku akieleza mafanikio yaliyopatikana pamoja na maeneo yanayohitaji kuimarishwa.
Vilevile, Postamasta Mkuu aliwapongeza wafanyakazi kwa mchango wao katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nane na Ule wa Mpito na kuwasihi kuendelea kufanya kazi kwa mshikamano, ubunifu na weledi ili kufanikisha malengo ya Shirika.

Kikao hicho kimekuwa hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya Posta Tanzania, kikionesha dhamira ya pamoja ya Bodi, Menejimenti na wafanyakazi katika kujenga Shirika la kisasa, lenye ushindani, linalotumia teknolojia na linalotoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wateja na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.

