JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

POSTA AFRIKA ZATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU


Taasisi za Posta Barani Afrika zaaswa kuongeza ubunifu na ufanisi katika utoaji wa huduma zake ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia sambamba na kuhakikisha huduma  zinazotolewa zinaakisi mahitaji ya wananchi kwa sasa.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Eng. Maryprisca Winfrend Mahundi wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) leo tarehe 11 Juni, 2024, katika Ofisi za Makao Makuu ya PAPU jijini Arusha.

Akifungua mkutano huo Mhe. Naibu Waziri amesisitiza Sekta za Posta Barani Afrika kuongeza ubunifu pamoja na kujikita zaidi katika utoaji wa huduma zake kidijitali hususani Biashara Mtandao “E-Commerce” ili kurahisisha huduma pamoja na kumpunguzia usumbufu mwananchi pindi anapohitaji huduma.

Aidha, Mhe. Inj. Maryprisca Mahundi ametumia nafasi hiyo kuupongeza Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kwa kuandaa vikao hivi vyenye lengo la kujadili maendeleo ya Sekta ya Posta Barani Afrika na kueleza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono shughuli zinazofanywa na Posta ili wananchi wanufaike na huduma hizo.

Naye kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nicholaus Merinyo Mkapa amesisitiza vikao vya PAPU vinavyoendelea vilete tija kwa ajili ya maendeleo ya Sekta za Posta Barani Afrika, kwa kuwa pasipo kupanga Kwa pamoja hapatakuwepo tena sababu ya kuwa pamoja.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika Dkt. Sifundo Chief Moyo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa jengo hilo la Makao Makuu ambapo sasa kwa mara ya kwanza PAPU inafanya vikao vyake kwenye jengo lake la Makao Makuu jijini Arusha.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA