JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

VIONGOZI WA POSTA AFRIKA WAZURU INDIA


Viongozi wa Posta za Afrika (Postamasta Wakuu na Wakurugenzi Wakuu) kwa nchi zinazoongea Kiingereza wamefanya ziara ya mafunzo nchini India kuanzia tarehe 21-26 Juni, 2024 ili kujionea namna India inavyofanya mageuzi ya Teknolojia katika uendeshaji wa Posta na kuhudumia wananchi wa nchi hiyo.

Ziara hiyo iliyoratibiwa na Umoja wa Posta Duniani, imefadhiliwa na Posta ya Marekani kwa kushirikiana na Posta ya India kupitia mpango wa Ushirikiano wa Kusini mwa Afrika (South-South and Triangular Cooperation-SSTC). 

Kwa upande wa Shirika la Posta Tanzania, Bi. Esther Epaphra, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango amemuwakilisha Postamasta Mkuu Bwana Maharage Chande. 

Katika ziara hiyo Bi. Esther ameambatana na Bw. Michael Njau, Mkurugenzi wa TEHAMA na Bw. Elia Madulesi, Mkuu wa Mawasiliano na Masuala ya Posta Kimataifa.

Ziara hiyo iliyoanzia jijini Mumbai na kuhitimishwa jijini Delhi ililenga kubadilishana uzoefu na viongozi hao katika masuala ya usimamizi na mifumo ya kiteknolojia pamoja na shughuli za Uendeshaji wa posta. Katika jiji Delhi viongozi hao wamejionea mageuzi mbalimbali yanayofanywa na Posta ya India ambayo mengi yanaweza kufanywa na posta za Afrika.

Viongozi wengine waliokuwepo katika ziara hiyo ni pamoja na wale wa nchi za Afrika Kusini, Botswana, Cameruni, Eswatini, Gambia, Ghana, Liberia ,Malawi Mauritius, Msumbiji, Kenya, Namibia, Rwanda , Seychelles, Nigeria, Sierra Leone, Zambia, Zimbabwe.

Wakitoa maneno ya mwisho ya kushukuru wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, “Mafunzo haya yalikuwa ni muhimu sana kwa viongozi wa Posta za Afrika kwa kuwa mazingira ya nchi ya India yanakaribiana sana na nchi za Afrika” Wamesema viongozi hao wakati wakitoa neno la shukrani kwa uongozi wa Posta ya India pamoja na UPU waliofanikisha ziara hiyo.  

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA