JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

POSTA AFRIKA ZAJIDHATITI KIDIJITALI


Sekta za Posta za nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) zimedhamiria kutoa huduma zake kidijitali sambamba na maendeleo ya Teknolojia yanayoendelea sasa Duniani huku zikitakiwa kutoa huduma stahiki na kwa kasi zaidi ili kukidhi mahitaji ya wananchi barani Afrika.

Hayo yalibainishwa jana tarehe 10 Juni, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa PAPU jijini Arusha, wakati wa jukwaa la Wakurugenzi Wakuu wa Posta na Taasisi za Udhibiti wa Mawasiliano (CEOs Forum) lililolenga kujadili na kupanga mipango ya maendeleo ya sekta ya Posta barani Afrika


Wakati wa jukwaa hilo mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo Utekelezaji wa mbinu mbalimbali za kidijitali ili kurejesha utoaji wa huduma za Posta baada ya janga COVID-19, na pia Usimamizi na Udhibiti wa huduma za kifedha za Posta zote zilizopo katika umoja huo.

Vilevile walijadili Gharama za Huduma za Posta 
sambamba na ushiriki wa mawazo na mbinu bora za kukuza huduma za Posta, Mambo Muhimu ya huduma za Kifedha za Posta ikiwemo Usalama wa mtandao, Miundombinu, Ugavi, Ushirikiano wa pamoja na Programu thabiti.

Aidha Tanzania ilipata nafasi ya kuwa mmoja wa watoa mada wakati wa jukwaa hilo ambapo Bw. Maharage Chande Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Posta za Afrika na huku akitoa wito wa kutumia maendeleo ya Teknolojia kama fursa katika kukuza huduma za Posta barani Afrika.

Sambamba na hilo, Bw. Maharage amewaasa nchi wanachama wa PAPU Kutokujifungia katika eneo moja na badala yake Posta zishirikiane katika kubadilishana uzoefu kama ilivyo kwa Posta Tanzania kwa sasa imejikita katika kushirikiana na Posta za Afrika katika kukuza Biashara Mtandao ambapo Posta ya Tanzania inamiliki Duka Mtandao linalowapa fursa wananchi na wafanyabiashara kupata huduma katika duka hilo.


Ikumbukwe kuwa Tanzania ni mwenyeji wa Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) ulioanza tarehe 3- 14 Juni, 2024 jijini Arusha yalipo Makao Makuu ya Ofisi za PAPU na kuhudhuriwa na wataalamu na wajumbe mbalimbali kutoka nchi wanachama wa PAPU pamoja na wadau  wa sekta ya Posta kutoka barani Afrika na Umoja wa Posta Duniani.Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA