JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

ANWANI ZA MAKAZI ZAIMARISHA HUDUMA


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari akimwakilisha  Mohammed Hamis Abdulla Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi unarahisisha utoaji wa huduma za posta na nyingine za kijamii, kuongeza uwajibikaji na kuridhika kwa wateja, huku ukichangia moja kwa moja maendeleo ya Teknolojia na huduma jumuishi za kifedha hasa kwa wananchi wa vijijini.

Dkt. Bakari alisema hayo leo katika siku maaalum ya Posta katika Kongamano la Mwaka la Anwani za Makazi na Maendeleo ya Teknolojia za huduma za Posta, kuwa teknolojia mpya, ikiwemo Vifaa Saidizi Binafsi vya Kidijitali (PDAs) vinavyotumiwa na wahudumu wa posta, vinawezesha kufikisha huduma kwa wateja kwa haraka na kwa usahihi. 

Aliongeza kuwa mafanikio ya Sekta hii yanahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na taasisi za kimataifa, kuhakikisha huduma za posta zinatumika kwa njia salama, bora na zinazomlenga raia.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa TPC Bw. Ferdinand Kabyemela akimwakilisha Macrice Mbodo, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania amesema kuwa kwa kuzingatia maazimio ya Umoja wa Posta Duniani (UPU) ambayo yanahimiza nchi wanachama kutumia mifumo sanifu ya Anwani za Makazi ambapo Shirika la Posta Tanzania limetekeleza maazimio hayo kwa ufanisi.

Bw. Kabyemela amefafanua kuwa mfumo huu unasaidia utoaji wa huduma kwa ufanisi, kupunguza gharama, kuongeza usalama wa barua na vifurushi, na kuunganisha wananchi na biashara katika uchumi endelevu. Mfumo huu pia unarahisisha upatikanaji wa mikopo, bima na huduma za kibenki, huku ukiwezesha huduma za Serikali kufikiwa haraka, ikiwemo afya, elimu, usalama na dharura.

Hata hivyo kupitia programu ya Posta Kiganjani, wateja wanaweza kuagiza bidhaa mtandaoni kupitia Kipepeo Shop na kuzipokea moja kwa moja majumbani kwao kwa kutumia anwani za makazi. Aidha, aliongeza kuwa TPC inalenga kujibadilisha kuwa Kituo Jumuishi cha Huduma za Posta (Postal Service Hub) kinachotoa huduma za posta, kifedha, kidijitali na huduma za Serikali, hususan kwa wananchi wa vijijini na pembezoni.

Naye Dr. Sifundo Chief Moyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), ameipongeza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za Afrika zilizothibitishwa kukidhi viwango vya kimataifa vya Anwani UPU S42, ambavyo vinarahisisha utambulisho wa Anwani na kuunganisha mifumo ya posta duniani kote . 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano la Afrika Mashariki (EACO), Bi.Caroline Koech, ameeleza kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa anwani za makazi, ambapo mpango wa Kitaifa umefanikiwa kufikia zaidi ya asilimia 95 ya nchi nzima. 

Aidha, amebainisha umuhimu wa uratibu wa kikanda kupitia majukwaa kama Jukwaa la Viongozi wa Posta wa Afrika Mashariki (EPLF) na Kikundi Kazi cha Masuala ya Posta, ambapo nchi washirika zinaweza kushirikiana uzoefu na kuendeleza mageuzi ya posta. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA