JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

BODI YATEMBELEA ENEO LA UJENZI DODOMA


Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania leo imetembelea eneo la Mtumba, mahali ambapo yanajengwa Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania, jijini Dodoma.

Ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya awali ya maandalizi ya ujenzi huo wa kimkakati, ambao unalenga kuimarisha uwepo wa Shirika kimuundo katika Makao Makuu ya Nchi, na kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya kisasa itakayowezesha utoaji wa huduma bora na za kisasa za Posta.

Wakiwa katika eneo hilo, Wajumbe wa Bodi walipata maelezo ya awali kuhusu hatua zilizochukuliwa katika maandalizi ya kiwanja, mipango ya usanifu wa jengo, na maono ya muda mrefu ya Shirika kuhusu ujenzi huo.

Aidha, *Bodi imemshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan*, kwa mchango wake mkubwa na kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu hayo kupitia Serikali ya Awamu ya Sita.  

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Tanzania Balozi Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi, akizungumza Kwa niaba ya Bodi amepongeza hatua hiyo ya kimkakati na kueleza kuwa ujenzi wa Makao Makuu hayo utaleta mageuzi makubwa katika utendaji wa Shirika kwa kuimarisha mazingira ya kazi, kukuza teknolojia, na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi kote nchini.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA