Habari
BUNGE LA BAJETI 2024/2025
HOTUBA YA WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI MHESHIMIWA NAPE MOSES NNAUYE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2024/25
UTANGULIZI
- Mheshimiwa Spika, Kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ambayo ilichambua Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Fungu 68) kwa Mwaka 2023/24, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako sasa likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2023/24. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka 2024/25.
Shukrani na Pongezi
- Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha sote kuwepo hapa kushiriki katika Mkutano huu wa kumi na tano wa Bunge la kumi na mbili.
- Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake madhubuti kwa kipindi cha miaka mitatu tangu aingie madarakani na kuendelea kutuongoza vyema huku tukishuhudia maendeleo na uwekezaji mkubwa kwa Sekta zote hususan Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Wizara inatambua matarajio makubwa aliyonayo Mheshimiwa Rais katika kufikishiwa huduma za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kama ilivyofafanuliwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025.
- Mheshimiwa Spika, Napenda pia kumpongeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango kwa namna anavyoendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuongoza nchi yetu kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi na Taifa kwa ujumla.
- Mheshimiwa Spika, vilevile nimpongeze Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kiongozi Mkuu wa shughuli za Serikali Bungeni, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), kwa miongozo na uongozi wake makini katika kulisimamia Bunge na Serikali kwa ujumla.
- Mheshimiwa Spika, Aidha, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb.) kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
- Mheshimiwa Spika, Vilevile, nikupongeze wewe binafsi kwa kuendelea kuliongoza Bunge lako Tukufu kwa weledi, busara, hekima na tija kusudiwa kwa kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa na ya wananchi yanajadiliwa kwa umakini. Pia, niendelee kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 31 wa Muungano wa Mabunge Duniani (IPU) na Baraza la Uongozi la IPU. Hakika unastahili pongezi za kipekee kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Bara la Afrika kushika wadhifa huo tangu historia ya kuanzishwa kwa chombo hicho. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.) Naibu Spika, kwa kuendelea kukusaidia kuliongoza Bunge lako. Nitumie fursa hii pia kuwapongeza Wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Dkt. Joseph Mhagama, Mbunge wa Madaba na Mheshimiwa Deo Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kwa kuchaguliwa kuliongoza Bunge lako Tukufu.
- Mheshimiwa Spika, naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Anne Kilango Malecela Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki na Wajumbe wa Kamati kwa ushirikiano wao kwangu na Wizara kwa ujumla katika kuhakikisha malengo ya sekta yanafikiwa. Pia ninaishukuru Kamati kwa kujadili kwa kina Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fungu 68, kwa Mwaka 2024/25 na kuyapitisha kwa kauli moja. Wizara imenufaika sana na umahiri, umakini na ushirikiano wa Kamati katika kuchambua, kushauri na kufuatilia majukumu yanayosimamiwa na Wizara. Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba maoni, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati yamezingatiwa kikamilifu katika Hotuba hii. Ninachoweza kuwaahidi kuwa maadam ‘imani huzaa imani’, mimi na wenzangu wizarani, tutakwenda kusimamia na kutekeleza maelekezo ya Kamati kikamilifu. Ninapenda kuwashukuru Watendaji wa Ofisi ya Bunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwa ushirikiano wao wakati wote ninapotekeleza majukumu yangu pamoja na wakati wa kuwasilisha taarifa mbalimbali kuhusu Wizara. Ninapenda kuwahakikishia kuwa, Wizara ninayoingoza itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili kufikia malengo ya Maendeleo ya Taifa na ya wananchi katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
- Mheshimiwa Spika, Nitumie fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Winfred Mahundi (Mb.) kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Ndugu Nicholaus Merinyo Mkapa kwa kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ninayoiongoza.
- Mheshimiwa Spika, kipekee na umuhimu mkubwa naomba nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Mtama kwa kuendelea kunipa ushirikiano wa dhati katika kujiletea maendeleo kwenye Jimbo letu; bila kuisahau familia yangu kwa upendo, uvumilivu katika nyakati zote ambazo nimekua nikiendelea kutekeleza majukumu yangu.
Salamu za Pole
- Mheshimiwa Spika, ninaomba nitumie fursa hii adhimu kutoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wanafamilia wote, Bunge lako Tukufu, ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa kuondokewa na kiongozi wetu Hayati Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika tutaendelea kumuenzi kwa umahiri wake na kwa mageuzi ya kisiasa aliyoyafanya, pamoja na kufungua nchi kiuchumi kwa kuruhusu uwekezaji wa sekta binafsi.
- Mheshimiwa Spika, vilevile, nitumie fursa hii kumpa pole Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanafamilia, ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa kuondokewa na Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowasa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hayati Lowassa ataendelea kukumbukwa kwa uthubutu wake, uwezo na ushawishi mkubwa katika kusimamia shughuli za Serikali.
- Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa natoa pole kwako Mheshimiwa Spika na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na wapendwa wetu Mheshimiwa Francis Leonard Mtega aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali kwa tiketi ya CCM na Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil aliyekuwa Mbunge wa Kwahani kwa tiketi ya CCM. Vilevile, naungana na Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla, kutoa pole kwa Watanzania wenzetu waliopatwa na majanga mbalimbali katika mwaka 2023/24, yakiwemo mafuriko na maporomoko ya mawe na matope katika maeneo ya Hanang Mkoani Manyara; Kibiti na Rufiji Mkoani Pwani pamoja na Malinyi, Ulanga, Ifakara, Mlimba Mkoani Morogoro na maeneo mengine nchini. Nipende kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Watanzania wote walioondokewa na wapendwa wao. Tunaomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.
Wajibu wa Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
- Mheshimiwa Spika, Wizara ina jukumu la kutunga na kusimamia Sera zinazohusiana na masuala ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuratibu na kusimamia vyombo vya Habari, Mawasiliano ya Posta na Simu; kuendeleza tafiti na ubunifu kwenye masuala ya TEHAMA; kuendeleza wataalam wa TEHAMA, kuanzisha na kusimamiana Postikodi, kuendeleza na kusimamia miundombinu ya Habari na Mawasiliano nchini ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Utekelezaji wa majukumu haya kutaiwezesha Tanzania kuimarika kushiriki uchumi wa kidijitali katika kufikia Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (4th, 5th na 6th Industrial Revolution) yanayochochewa na kuwezeshwa na matumizi ya TEHAMA ambayo yatasaidia kuwa na jamii inayopata taarifa sahihi kwa wakati ili wananchi waweze kushiriki katika kuleta maendeleo.
- Mheshimiwa Spika, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Fungu 68) inasimamia Taasisi tisa ambazo zimegawanyika kwenye umahsusi wa Huduma, mashirika ya kibiashara, udhibiti, mfuko, baraza na taasisi wezeshi. Taasisi hizo ni: Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania; Shirika la Mawasiliano Tanzania; Shirika la Posta Tanzania; Shirika la Utangazaji Tanzania; Kampuni ya Magazeti ya Serikali; Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote; Tume ya TEHAMA; Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano. Hotuba hii itaelezea kwa ufupi masuala yanayotekelezwa na Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Hali ya Ukuaji wa Sekta ya Habari na Mawasiliano na Upatikanaji wa Mawasiliano Nchini
- Mheshimiwa Spika, Sekta ya Mawasiliano imeendelea kukua ambapo takwimu zinaonesha kuwa laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 62.3 Mwezi Aprili, 2023 hadi kufikia laini milioni 72.5 Mwezi Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 16.4. Watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 33.1 Mwezi Aprili, 2023 hadi kufikia milioni 36.8 Mwezi Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 11.2. Watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya mtandao wa simu wameongezeka kutoka milioni 44.3 mwezi Aprili, 2023 hadi kufikia Milioni 53.0 mwezi Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 19.6. Aidha, Watoa huduma wa Miundombinu ya Mawasiliano wamefikia 25 ukilinganisha na watoa huduma 23 Mwezi Aprili, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 8.7.
Hatua iliyofikiwa ya Mapinduzi ya Uchumi wa Kidijitali
- Mheshimiwa Spika, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ina wajibu wa kusimamia Mapinduzi ya Kidijitali nchini. Mapinduzi ya Kidijitali yanaweka msingi wa kulipeleka Taifa kwenye Uchumi wa Kidijitali unaowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA. Katika Uchumi wa kidijitali, Sekta zote hufanya kazi kwa pamoja, kwa ushirikiano na muingiliano zikiwezeshwa na mazingira bora ya kidijitali. Ili kuharakisha Tanzania kuelekea katika uchumi wa kidijitali, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanza kutumika kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Kanuni zake pamoja na uanzishwaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Hatua hii ni muhimu hasa ukizingatia kuwa mapinduzi ya kidijitali yanachochewa na matumizi ya taarifa (Data) ambayo imekua ni bidhaa adimu. Pia Serikali imepitisha Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Kidijitali 2024-2034 utakaosaidia kuongeza matumizi ya kidijitali kwa huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na Sekta binafsi. Mkakati huo una nguzo muhimu sita (6) zikiwemo uwezeshaji wa miundombinu ya Kidijitali, utawala wa Kidijitali na uwepo wa Mazingira wezeshi, kujenga uelewa na ukuzaji wa ujuzi wa kidijitali, uwepo wa utamaduni wa ubunifu wa kidijitali na teknolojia wezeshi, tamaduni ya ujumuishaji wa makundi maalum katika matumizi ya kidijitali na kuwezesha huduma za kifedha kwa kidijitali pamoja na maamuzi ya Serikali ya kuihamishia Mamlaka ya Serikali Mtandao kuwa moja ya Taasisi chini ya Wizara. Hatua hii itawezesha kuchochea ukuaji wa matumizi ya TEHAMA pamoja na ujenzi wa mifumo mbalimbali ya utoaji huduma kwa mujibu wa malengo na mwelekeo wa kisera. Katika hatua hii tunamshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Baraza la Mawaziri.
- Mheshimiwa Spika, Katika safari hii ya mapinduzi ya kidijitali Wizara imeanza kufanya marejeo ya Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 pamoja na kuandaa 14 ya miongozo mbalimbali itakayotumika katika usimamizi wa Sekta ya TEHAMA ambayo itasaidia kuboresha utendaji kazi wa Taasisi kwa kutumia mifumo ya kidijitali, kuifanya Tanzania kuwa na viwango vinavyotambulika kimataifa katika TEHAMA, usimamizi wa misingi ya mageuzi ya kidijitali nchini, kujenga uelewa kwa wananchi wote kuhusu matumizi ya TEHAMA, ujumuishaji wa makundi ya anuai katika huduma za kidijitali, matumizi ya akili mnemba, Mkakati wa Usalama Mtandao (Cyber Security Strategy) pamoja na Mkakati wa Kufanya Tafiti na Bunifu za TEHAMA nchini.
- Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Tanzania inapiga hatua zaidi katika uchumi wa Kidijitali, Wizara kwa kushirikiana na wadau muhimu inaendelea kuandaa mfumo jumuishi (Samia’s Technology Stack) unaojumuisha mifumo mitatu (3) ambayo ni: Mfumo wa Jamii Namba ambao utatumika kufanya utambuzi wa kipekee wa kila mwananchi kuanzia anapozaliwa ambapo atakuwa na akaunti ya kidijitali itakayomwezesha kupata huduma zote za kijamii; Mfumo wa Jamii Malipo ambao utawezesha wananchi kutumia Jamii Namba kupokea fedha na kurahisisha kufanya malipo kidijitali. Mfumo huu pia utasaidia Financial Inclusion na kuongeza Wigo wa mapato ya Serikali; na Mfumo wa Jamii Data Shirikishi ambao unamwezesha mwananchi kumiliki taarifa zake katika kupokea huduma mbalimbali nchini. Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao na Tume ya TEHAMA Nchini imeanza ujenzi wa Mfumo wa Ubadilishanaji taarifa uitwao Jamii Data Exchange Platform/ Tanzania Enterprise Service Bus.
Hali ya Sekta ya Habari Nchini
- Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha Sekta ya habari nchini ambapo vituo vya kurusha matangazo ya runinga vimeongezeka kutoka vituo 65 mwaka 2023 na kufikia vituo 68 Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 4.6 na Cable Television zimeongezeka kutoka 57 Aprili, 2023 na kufikia 60 Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 5.3. Vituo vya kurusha matangazo ya redio vimeongezeka kutoka vituo 215 mwaka 2023 hadi kufikia vituo 231 Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 7.4 na magazeti yameongezeka kutoka 321 Aprili, 2023 na kufikia 351 Aprili, 2024 sawa na ongezeko la 9.3. Aidha, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya teknolojia za utangazaji hasa maudhui mtandaoni ambayo pia yamechangia kuongeza ajira kwa vijana.
Uhuru wa vyombo vya habari
- Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuhakikisha kuwa vyombo vya habari nchini vinakuwa huru kupokea na kutoa habari za matukio mbalimbali yanayojitokeza katika jamii. Takwimu kutoka World Press Freedom Index 2024 inayoratibiwa na Taasisi ya Reporters without boarders (RWB)(RSF) zimeonyesha kuwa Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kuheshimu uhuru wa habari, ambapo Kimataifa imeshika nafasi ya 97 Mwaka 2024 toka nafasi ya 142 Mwaka 2023 na kupelekea kupanda katika kuheshimu uhuru wa vyombo vya Habari. Mafanikio haya yametokana na Serikali kuchukua hatua muhimu ikiwemo Bunge lako Tukufu kufanya mabadiliko ya sheria ya huduma ya vyombo vya habari 2016 Mwaka 2023.
Gharama za Mawasiliano ya Simu
- Mheshimiwa Spika, Takwimu zinaonesha kuwa wastani wa bei ya dakika ndani ya mtandao bila kifurushi (Shilingi/dakika) zimeendelea kushuka kutoka Shilingi 29.0 Juni, 2023 hadi kufika wastani wa Shilingi 26.00 Aprili, 2024, wakati bei ya dakika nje ya mtandao bila kifurushi imeshuka kutoka wastani wa Shilingi 31.0 Juni, 2023 hadi kufikia wastani wa Shilingi 28.00 Machi, 2024. Mwenendo wa gharama za rejareja za data bila kifurushi na kwenye kifurushi zimeendelea kupungua. Aidha, katika robo ya mwaka inayoishia Machi 2024, gharama za data ndani ya kifurushi zimeshuka na kufikia wastani wa Shilingi 2.17 kwa Mb Aprili, 2024 ikilinganishwa na Shilingi 2.25 kwa Mb Juni, 2023.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA NA TAASISI ZAKE KWA MWAKA 2023/24
Bajeti iliyoidhinishwa
- Mheshimiwa Spika, Katika Mwaka 2023/24 Wizara iliidhinishiwa kutumia kiasi cha Shilingi bilioni 212.4. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 30.5 ziliidhinishwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi bilioni 18.5 ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi bilioni 11.9 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Aidha, Shilingi bilioni 181.9 ziliidhinishwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, ambapo Shilingi bilioni 146.8 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 35.2 ni fedha za nje.
Fedha zilizopokelewa na Wizara
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 Wizara imepokea jumla ya Shilingi bilioni 213.9 sawa na asilimia 100.7 ya Shilingi bilioni 212.4 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge katika Mwaka 2023/24. Kati ya fedha zilizopokelewa Shilingi bilioni 16.3 ni kwa ajili ya Mishahara, Shilingi bilioni 7.0 ni Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni 190.6 ni fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Fedha za miradi ya maendeleo inajumuisha Shilingi bilioni 102.1 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 88.5 ni fedha za nje.
MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2023/24
- Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tumefanikiwa kutekeleza yafuatayo:
- Kufanya tathmini ya hali ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 na Sera ya Taifa ya Mawasiliano ya Simu ya mwaka 1997 na kuandaa Rasimu ya Sera Mpya ya Taifa ya TEHAMA 2024;
- Kuandaa Rasimu ya Sera ya Kampuni changa za TEHAMA (Startups);
- Kuanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambayo ilizinduliwa tarehe 3 Aprili, 2024 na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
- Kukamilisha kuhamisha shughuli zote za Ujenzi na uendeshaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Kituo cha Kuhifadhi Data (NIDC) kwenda Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL);
- Kukamilisha ujenzi wa Kilomita 3,008 na Vituo 66 vya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano;
- Kukamilisha upanuzi wa Mkongo wa Taifa kutoka ukubwa wa 200Gbps kwenda 800Gbps kwenye mizunguko mikuu ya Mkongo wa Taifa na kuanza upanuzi wa Mkongo kutoka 800Gbps hadi 2000Gbps;
- Kuanza Ujenzi wa minara 758 katika Kata 731 na kuongeza uwezo wa minara 304 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 2G/3G na 4G. Hadi Aprili, 2024 Minara 142 imekamilika kujengwa ambapo minara 124 tayari inatoa huduma. Aidha, minara 243 imeongezewa nguvu;
- Kukamilisha Ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na kuzinduliwa rasmi tarehe 2 Septemba 2023 na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Arusha;
- Kukamilisha Ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kuzinduliwa rasmi tarehe 25 Aprili, 2024 na Dkt. Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Dodoma;
- Kukamilisha ujenzi wa miradi ya upanuzi wa usikivu wa redio za TBC katika maeneo saba ya Serengeti – Mara, Bariadi – Simiyu, Ileje – Songwe, Njombe, Kilwa – Lindi, Unguja na Pemba;
- Kukamilika, kuridhiwa na kuanza kutumika kwa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali 2024 – 2034 na Miongozo sita ya Usimamizi wa Sekta ya TEHAMA;
- Kukamilisha majadiliano kati ya Serikali na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano (consortium) kulikopekelea Serikali kulipwa Dola za Marekani milioni 33;
- Kusainiwa kwa Mikataba ya mauzo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na nchi za Uganda wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 28.8, Malawi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5.5, Burundi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 3.3 na Kampuni ya Airtel wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4.8;
- Kuunda Kamati ya Kitaifa ya usimamizi wa Setelaiti nchini kwa ajili ya kuratibu, kusimamia na kuendeleza shughuli za anga za juu nchini;
- Kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya TBC katika eneo la Vikonje Jijini Dodoma ambapo hadi Aprili, 2024 ujenzi umefikia asilimia 18;
- Kuanza ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya kufunga mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji ambapo ujenzi umefikia asilimia 35;
- Kuongeza Ushiriki wa Tanzania kwenye masuala ya kikanda na kimataifa hasa kwa Mashirika hususani Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU), Shirika la Mawasiliano Afrika (ATU), Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umoja wa Posta Duniani (UPU);
- Kushinda tuzo ya ubora kwa Shirika la Posta Tanzania kutokana na kuandaa, kusimamia na kutekeleza miradi inayofadhiliwa na Umoja wa Posta Duniani;
- Kupata obiti mpya ya setelaiti ya 160W kwa matumizi ya Satelaiti za Utangazaji na masafa mapya yatakayotumika katika kuboresha usalama wa mawasiliano ya angani na majini;
- Kuwezesha kupungua kwa gharama za uwekaji wa miundombinu ya mawasiliano kwenye hifadhi za barabara ambapo ada ya awali imepungua kutoka Dola za Marekani 1000 hadi 200 kwa Kilomita na Ada ya mwaka imepungua kutoka Dola za Marekani 1000 hadi 100 kwa Kilomita;
- Kuwezesha ujenzi na uzinduzi wa Kituo cha Mkongo wa Baharini wa 2Africa wenye uwezo wa kusukuma kiwango kikubwa cha intaneti kuanzia 17Tbps hadi 180Tbps;
- Kuunganisha ofisi 50 za RUWASA kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano;
- Kuunganisha watumiaji 12,584 na huduma za faiba mlangoni;
- Kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Kituo cha kuhifadhi data Zanzibar;
- Kuhakiki na kuboresha taarifa za Anwani za Makazi katika Halmashauri tano (5) ambazo ni Manispaa za Morogoro, Iringa, Singida, Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Mji wa Masasi. Kupitia zoezi hili Anwani 2,308,231 (Tanzania Bara 1,937,111 na Zanzibar 371,120) zimehakikiwa kati ya anwani 12,385,956 zilizokusanywa wakati wa operesheni. Vilevile, Anwani mpya 505,436 zimesajiliwa na kufanya idadi ya Anwani za Makazi zilisosajiliwa kuongezeka hadi 12,891,392 sawa na ongezeko la asilimia 4.1;
- Kufanya maboresho ya mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) kuwezesha kutoa barua za utambulisho wa ukaazi kupitia Watendaji wa Kata na Shehia kidijitali. Moduli hii imezinduliwa Aprili 2024 kwa majaribio ambapo hadi sasa jumla ya barua 708 kutoka mitaa 152 zimeombwa na kutolewa;
- Kutoa ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 20 wa Serikali katika nchi za Ujerumani, Uingereza, Malaysia na Marekani. Aidha, Serikali imetangaza nafasi nyingine 480 za mafunzo ya muda mfupi kupitia mradi wa Tanzania ya kidijitali;
- Kudhibiti mawasiliano ya simu ambapo simu za ulaghai 767 zimebainika na hatua stahiki zimechukuliwa kwa mujibu wa Sheria;
- Kuanza utekelezaji wa mradi wa Muundombinu wa Kitaifa wa Saini za Kielektroniki (NPKI);
- Kukamilisha ujenzi wa maabara ya uidhinishaji wa vifaa vya mawasiliano ya kieletroniki (type approval laboratory), ambao unajumuisha maabara ya kupima mionzi inayotokana na simu za mkononi (specific absorption rate lab) na maabara ya kupima masafa ya kifaa (radio frequency lab)
- Kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Miji Janja (Smart Cities) katika Majiji ya Dodoma, Arusha na Mbeya;
- Kupeleka huduma ya Wi-Fi uwanja wa Benjamin Mkapa, Viwanja vya sabasaba, Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CoICT) Kijitonyama na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM);
- Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa majukumu mengine ya Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA yameainishwa kwenye Ukurasa wa 19 hadi 42 wa kitabu cha hotuba ya bajeti.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushirikisha Sekta Binafsi katika utekelezaji wa majukumu yake ambapo katika mwaka 2023/24 Sekta binafsi zimeendelea kushirikiana na Wizara katika maeneo yafuatayo:
- Hati ya mashirikiano kati ya Serikali na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano (Consourtium of Telco Operators) imefanyiwa maboresho na kusaini. Matokeo ya ushirikiano huu ni kujengwa kwa miundombinu ya Mkongo wa Mawasiliano katika Maeneo ambayo Mkongo wa Taifa haujafika na miundombinu hiyo iliyokamilika inatarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali ili kujumuishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano;
- Kampuni tano za Mawasiliano ya Simu zimechangia asilimia 60 ya gharama za ujenzi wa Minara 758 katika Kata 713 inayoendelea kujengwa sehemu mbalimbali nchini;
- Utoaji wa huduma ya intaneti kwenye maeneo ya wazi;
- Utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi na salama ya mawasiliano;
- Kuendelea kuanzisha televisheni na redio kwa lengo la kuwezesha kuhabarisha umma na kuharakisha bunifu za kidijitali; na
- Tumefanikiwa kuwezesha kusainiwa kwa hati ya ushirikiano kati ya Kampuni ya Airtel Tanzania na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kuunganisha Shule 3,000 na mtandao wa intaneti kwa kipindi cha miaka mitano.
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2024/25
- Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa Mpango na Bajeti wa mwaka 2024/25 kwa kuzingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025; Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26); na Hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akihutubia Bunge tarehe 22 Aprili, 2021.
Makadirio ya Mapato ya Wizara
- Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2024/25, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Fungu 68) inakadiria kukusanya kiasi cha Shilingi 100,700,000,000 ambazo zitatokana na mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, usajili wa Magazeti, ada ya mwaka ya Magazeti, vitambulisho vya Waandishi wa Habari na machapisho ya picha, mabango na majarida.
Malengo ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
- Mheshimiwa Spika, Wizara inasimamia Mapinduzi ya Kidijitali yanayowezeshwa na TEHAMA na pia kuimarisha mfumo wa kupashana habari kwa kusimamia uhuru wa vyombo vya habari nchini. Mapinduzi ya Kidijitali ndio yanayoweka Msingi wa kulipeleka Taifa kwenye Uchumi wa Kidijitali unaowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA. Ili kuwezesha mageuzi na mapinduzi haya kwenye Sekta zote za Uchumi na Kijamii, Wizara kwa kushirikiana na Sekta binafsi imepanga kufanya mabadiliko na maboresho makubwa kwenye Sekta ili kuendana na mageuzi kwa kutunga na kuhuisha Sera, Sheria na Miongozo inayosimamia Sekta za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na Posta kote nchini, kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza na kuimarisha Biashara Mtandao nchini, kuimairisha miundombinu itakayowezesha utekelezaji wa uchumi wa kidijitali, kuimarisha ulinzi na usalama wa anga ya mtandao, kuimarisha upatikanaji wa habari nchini, na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuchochea ubunifu na kuimarisha ustawi wa kampuni changa (Startups).
- Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2024/25 Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo:
- Kukamilisha uhuishwaji wa Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003, Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 na kutunga Sera mpya ya Taifa ya TEHAMA ambayo itajumuisha masuala ya Kampuni changa za TEHAMA (Startups);
- Kuratibu utungwaji wa Sheria ya Anwani za Makazi;
- Kufanya mapitio ya Sheria ya usalama wa mtandao ya mwaka 2015 ili iendane na wakati wa sasa na pia iweze kujumuisha masuala ya kumlinda mtoto dhidi ya ukatili wa mtandaoni na masuala ya ugaidi mtandaoni;
- Kukamilisha ujenzi wa minara ya mawasiliano ya Simu 616 ili kuweza kufikia minara 758 katika kata 713 pamoja na kuanza ujenzi wa minara mingine mipya 636 ili kuhakikisha maeneo yaliyobakia yanapata mawasiliano.
- Kuiongezea nguvu minara 135 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 2G/3G na/au 4G;
- Kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo 70 ya kimkakati mathalan maeneo ya hifadhi na mipakani;
- Kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye Wilaya 40 nchini;
- Kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Ziwa Tanganyika;
- Kuanza ujenzi wa Kituo cha Kuhifadhi Data Dodoma na Zanzibar pamoja na kuanzisha Kituo kimoja cha Usalama wa Mawasiliano cha Taifa;
- Kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na vyombo vya ulinzi na usalama (Mahakama, TAKUKURU, Polisi, Magereza, JWTZ, Usalama) pamoja na taasisi 100 za Haki Jinai na Taasisi nyingine za Serikali;
- Kuendelea kuimarisha mifumo ya kusimamia na kupima ubora wa huduma za mawasiliano ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma na usimamiaji wa Sekta;
- Kuwezesha Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) kuunganishwa na mifumo mingine ya kutolea huduma za kijamii;
- Ununuzi wa magari mawili maalumu ya kurushia matangazo mbashara (OB Van) na magari 15 kwa ajili ya shughuli za utangazaji katika vituo vipya vya kurushia matangazo ikiwemo kuwezesha kutangaza shughuli za Uchaguzi Mkuu na wa Serikali za Mitaa;
- Kuendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, Baraza Huru la Habari na Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari;
- Kuratibu uanzishaji wa Wakala wa Anga za Juu nchini (Tanzania Space Agency) na kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Anga za Juu (Outer Space Strategy);
- Kutengeneza na kutumia mfumo wa kukusanya na kusambaza mizigo (“uberlike” pick and delivery system);
- Kusimamia uundaji wa mfumo wa kidijitali utakaowezesha biashara Mtandao (e-Commerce);
- Kutekeleza mradi wa kujenga kituo cha kikanda kitakachojumuisha maghala maalum ya kuhifadhi bidhaa, huduma ya ugomboaji na ushuru wa forodha ili kuwezesha biashara mtandao;
- Kuendelea kusimamia utekelezaji wa Muundombinu wa Kitaifa wa Saini za Kielektroniki (NPKI) ili kuhakikisha usalama wa miamala ya kielektroniki nchini;
- Kuendelea na uratibu wa uendelezaji wa Mifumo ya Kitaifa nchini;
- Kujenga maabara za Akili Mnemba (AI) na matumizi ya Roboti nchini;
- Kuendelea kuwezesha uanzishaji na ukuzaji wa vituo vya ubunifu vya TEHAMA katika Wilaya sita (6) kwa kuanzia (District ICT Startups Innovation hubs);
- Kuwaendeleza wataalam 30 wa TEHAMA kwenye programu za muda mrefu na wataalam 450 kwenye programu za muda mfupi;
- Kuanza ujenzi wa vyuo viwili (2) vya TEHAMA Nala - Dodoma na Buhigwe - Kigoma;
- Kusajili wakusanyaji na wachakataji 500,000 wa taarifa binafsi;
- Kuendelea kuimarisha usikivu wa redio za TBC kwa kujenga mitambo ya redio yenye masafa ya FM kwenye Wilaya saba za Buhigwe, Malinyi, Lushoto, Buchosa, Mafia, Ikungi na Kaliua; na
- Kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha uchapaji na kufunga mitambo ya kisasa ya uchapaji.
- Mheshimiwa Spika, Mipango mingine ya Sekta ya Mawasiliano imefafanuliwa katika Ukurasa wa 43 hadi 57 wa kitabu cha hotuba ya bajeti.
Mchango wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25
- Mheshimiwa Spika, katika kuunga mkono juhudi za Serikali, kwa mwaka 2024/25 Sekta Binafsi imeridhia kutekeleza yafuatayo:
- Kampuni za simu za Airtel Tanzania, Vodacom Tanzania, Honora Tanzania, Halotel na TTCL yamepanga kuendelea kushirikiana na Serikali kwenye ujenzi wa minara 616 ya mawasiliano ya simu kati ya minara 758 na kuendelea kuongeza uwezo kwenye minara 61 kati ya minara 304. Aidha, kampuni hizi zimepanga kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa minara mipya 636 ya mawasiliano ya simu;
- Kampuni ya simu ya Airtel Tanzania imepanga kupeleka huduma ya Wi-Fi katika maeneo 16 kati ya 120 yaliyopendekezwa na Wizara kwa Mwaka 2024/25. Maeneo yatakayofikishiwa huduma ni: Vyuo, Masoko, Hospitali, Vituo vya mabasi na Stesheni za treni ya mwendokasi;
- Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – MISA, imepanga kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano nchini; na
- Kushirikiana na Serikali katika kukuza bunifu za TEHAMA na kukuza kampuni changa za TEHAMA.
SHUKURANI
- Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati ninapenda kuwashukuru wale wote walioshiriki kunisaidia kutekeleza majukumu yangu katika Wizara hii. Kipekee niwashukuru Mheshimiwa Maryprisca Winfred Mahundi (Mb.), Naibu Waziri; Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu na Nicholaus Merinyo Mkapa, Naibu Katibu Mkuu. Aidha, nawashukuru Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo katika Wizara, Wenyeviti wa Bodi za Wakurugenzi za Taasisi zilizo chini ya Wizara; Viongozi wa Taasisi na wafanyakazi wote wa Wizara na Taasisi kwa kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa Wizara yetu inakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia Habari na TEHAMA.
- Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kipekee kuwashukuru Washirika wa Maendeleo ambao Serikali imekuwa ikishirikiana nao katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazohusiana na Sekta za Habari na Mawasiliano. Washirika hao ni: Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU); Shirika la Umoja wa Posta Duniani (UPU); Shirika la Umoja wa Posta Afrika (PAPU); Benki ya Dunia (WB) kupitia dirisha la Wakala wa Maendeleo ya Kimataifa (IDA), Ubalozi wa Korea Kusini nchini na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).
- Mheshimiwa Spika, ningependa pia kuzishukuru Jumuiya za Kikanda na Kimataifa za Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Ulaya (EU) kwa ushirikiano katika masuala ya Kikanda na Kimataifa yanayohusu Sekta hii. Aidha, Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inachangia katika kutimiza Dira ya Taifa ya kufikia Uchumi wa Kati wa Juu ifikapo Mwaka 2025. Kwa upekee niyatambue makampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania, Airtel Tanzania, Honora Tanzania, Halotel, TISPA na TTCL kwa kusambaza huduma za mawasiliano nchini. Vilevile, napenda kuzitambua taasisi za kifedha ikiwa ni pamoja na benki ya CRDB, NMB, TSA kwa mchango wao katika kukuza bunifu za TEHAMA nchini. Pia napenda kuvishukuru vyombo vya Habari vyote pamoja na Jumuiya zake ikiwemo MOAT, TAMWA, MCT, UTPC, MISA Tan, TADIO, TMF, TEF, JOWUTA, JUMIKITA na Jamii Forums kwa kuendelea kuhabarisha umma. Kwa kumalizia natambua mchango wa wadau wote wa Sekta ikiwemo Kampuni ya Minara Tanzania, Herios Tower, Huawei, Softnet, Telecom Associate, TanzTech pamoja na Raddy Fibre.
MUHTASARI WA MAOMBI YA FEDHA YA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI KATIKA MWAKA 2024/25
- Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2024/25, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni mia moja themanini, milioni mia tisa ishirini na sita, mia tano hamsini na saba elfu kwa mchanganuo ufuatao:-
- Kiasi cha Shilingi bilioni thelathini na nane, milioni mia tisa na sita, mia sita sitini na tatu elfu ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi bilioni ishirini na nne, milioni mia tisa tisini na saba, mia nne sabini na nne elfu ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi bilioni kumi na tatu, milioni mia tisa na tisa, mia moja themanini na tisa elfu ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo; na
- Kiasi cha Shilingi bilioni mia moja arobaini na mbili, milioni kumi na tisa, mia nane tisini na nne elfu kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi bilioni mia moja kumi na sita, milioni mia nne sitini na tisa, mia nane tisini na nne elfu ni Fedha za Ndani na Shilingi bilioni ishirini na tano, milioni mia tano hamsini ni Fedha za Nje.
- Mheshimiwa Spika, hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara ambayo ni http://www.mawasiliano.go.tz.
- Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.