Habari
CHANDE AKUTANA NA MKURUGENZI MKUU UPU
02 Mei, 2024
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) Bwana Masahiko Metoki wakati wa vikao vya Baraza la Utawala la Umoja huo vilivyoanza tarehe 29 April hadi 3 Mei, 2024 jijini Berne, Uswis.
Pamoja na mambo mengine Postamasta Mkuu amemshukuru Bwana Metoki kutokana na misaada ya kiufundi inayotolewa na Umoja huo ikiwemo mafunzo mbalimbali ya kuimarisha Utendaji katika sekta ya Posta ikiwemo mafunzo ya Usafirishaji, Utayari wa kufanya Biashara Mtandao, Utumaji wa Taarifa za Awali za Kielektronik, Uboreshaji wa huduma za EMS na Utayari wa kutoa huduma wakati wa Majanga.
Pia ametumia nafasi hiyo kumshukuru Bwana metoki kwa vifaa mbalimbali ambavyo Shirika la Posta Tanzania limepokea kutoka UPU ikiwemo Pikipiki 22, Skana 127, Kompyuta Mpakato 8, Kumpyuta za mezani 24, Kamera za Ulinzi 10, tablet 2 Printer 2 na Simu za Mkononi 2.
Aidha, Bwana Maharage ameshukuru Umoja huo chini ya Bwana Metoki kwa kuiamini Tanzania kuendesha Ofisi ya Miradi kwa Ukanda wa Afrika ya Mashariki pamoja na kituo cha kutegemeza Teknolojia kwa nchi zinazoongea kiingereza na msumbiji vyote vikiendeshwa na watumishi wa Shirika la Posta Tanzania.
Kwa upande wake Bwana Metoki amepongeza mageuzi yanayoendelea kufanywa na Shirika la Posta Tanzania ambayo yana lengo la kuendana na mahitaji ya wateja yanayobadilika kwa haraka huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa Tanzania kila itakapohitajika.
Katika mazungumzo hayo Bwana Maharage aliambatana na Bwana Mulembwa Mnaku, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Cecilia Mkoba, Meneja Huduma za Posta- Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania; Bw. Constantine Kasese, Mkurugenzi, Biashara Mtandao na Uwakala wa Fedha(TPC), Elia PK Madulesi, Meneja wa Uhusiano (TPC)
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano
Shirika la Posta Tanzania