JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

HUDUMA ZA KIFEDHA NJE YA MIPAKA


Shirika la Posta Tanzania limejidhatiti kikamilifu katika utoaji wa huduma za kifedha ndani na nje ya nchi kwa kutumia huduma za Kimataifa kama vile MoneyGram, WestenUnion na International Financial Services-IFS kwa lengo la kuendelea kuwafikia wananchi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Hayo yamethibitika tarehe 21 Machi, 2024 wakati Mkurugenzi wa Biashara Mtandao na Huduma za Fedha na Uwakala Bw. Constantine Kasese akiwasilisha kwa niaba ya Postamasta Mkuu kuhusu Mpango na Mkakati na Mwelekeo wa Shirika hususani katika huduma za fedha katika Kikao kazi cha Kujengeana Uwezo wa Utoaji wa Huduma za Fedha Kuvuka Mipaka (Cross Border Remittance) katika Hoteli ya Urban City Blue, jijini Dar es Salaam.

Kikao kazi hicho cha siku tatu kuanzia tarehe 20-22 Machi, 2024 kilichoandaliwa na FINSYS Tanzania Ltd kwa kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania kina lengo la kuangalia nafasi ya Shirika la Posta Tanzania katika kutoa huduma za Fedha kwa kuvuka Mipaka kwa kutumia fursa ya Mtandao mpana wa Shirika la Posta ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa zaidi ya ofisi 251 ndani na ofisi 670,000 duniani.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Taasisi ya FINSYS, Shirika la Posta Tanzania, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Benki Kuu (BOT), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wizara ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (WMJJWM), ZimPost na EuroGiro pamoja na Taasisi ya SendHome kutoka Afrika ya Kusini.

Mada mbalimbali toka kwa wasimamizi na wadhibiti wa sekta ya fedha na mawasiliano (BOT na TRCA), Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), Wizara ya Habari, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Posta Zimbabwe (ZimPost), EuroGiro pamoja na Taasisi ya SendHome ziliwasilishwa kwa ajili ya kuwezesha Shirika la Posta kuwa Mtoa huduma za Fedha kwa njia za Kisasa na zenye tija kwa wananchi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Aidha mada hizo zilitolewa kwa kuzingatia Sheria, Taratibu Kanuni na Mifumo ya Wasimamizi wa sekta ya Fedha kwa ajili ya kuhakikisha usalama na uhakika wa huduma zinazotolewa.

Maazimio ya kikao kazi hiki ni kulijengea uwezo Shirika la Posta Tanzania kuwa na huduma za kifedha zinazovuka mipaka kwa kutumia mifumo ya kisasa ya serikali na kutengeneza mpango kazi wa kuzifikia nchi nyingi katika kanda za EAC, SADC na COMESA hadi kufikia mwaka 2025

Imetolewa na;  Kitengo cha Uhusiano

                        Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA