JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

POSTA KIDIJITALI KURAHISISHA HUDUMA



 Dodoma 

KATIBU Mkuu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amelitaka Shirika la Posta Tanzania kuwa na mifumo rafiki ya kidijitali inayosomana ili kurahisisha huduma kwa wateja na kulifanya Shirika kuwa na urahisi wa kuwahudumia wateja wengi kwa wakati na kwa ufanisi. 

Ameyasema hayo leo Julai 12, 2024 wakati akishuhudia makabidhiano ya vifaa saidizi vya kidijitali( Personal Digital Assistant-PDA) vipatavyo 250  ambavyo vinasaidia kupokea, kusafirisha na kufikisha taarifa za bidhaa za wateja kwa wakati. Vifaa hivyo vimetolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa Shirika la Posta Tanzania. 

Wakati wa makabidhiano hayo Bw. Abdulla amesema huduma zikitolewa ni lazima mifumo  isomane ili kuondoa usumbufu kwa mteja na Shirika, na kupunguza usumbufu wa kutumia mifumo mbalimbali kukamilisha utaratibu wa mteja husika.

"Mfanyakazi wa Posta mwenye PDA anapopeleka bidhaa kwa mteja, taarifa zitumwe kutoka huko aliko. Ule mtirirriko wa tangu mteja ananunua na kusafirishiwa hadi kufikishiwa bidhaa yake  ndio maana halisi ya mifumo kusomana, ili hata inapotengenezwa taarifa ni rahisi kuuona mtiririko wa aina moja badala ya kutafuta taarifa kwenye mifumo tofauti tofauti" alieleza Bw. Abdulla. 

Aidha, aliongeza kuwa anatarajia kuona Shirika la Posta likiendelea kuwa bunifu, likitoa huduma zake kwa njia za kisasa za kidijitali kwa wateja wa ndani na nje ya nchi.

Wakati wa hafla hiyo Bw. Abdulla alionesha kufurahishwa na mabadiliko makubwa ya kidijitali yanayofanywa na Shirika hilo yenye kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.

 

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania,  Brigedia Jenerali Mstaafu Yohana Ocholla Mabongo, alieleza kuwa vifaa hivyo vitakwenda kuleta chachu ya utendaji kazi na kuongeza kasi ya kutekeleza shughuli za Posta kidijitali kwa kuwa tunaposema Posta kidijitali na vifaa vyake viendane na mlengo wa Shirika kidijitali. 

 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Bi. Justina Mashiba alieleza kuwa Mfuko huo umewezesha kwa kiasi kikubwa upande wa mawasiliano ya simu na sasa wameona ni wakati muafaka wa kuongeza nguvu zaidi katika mawasiliano ya Posta na usafirishaji wa Posta kwa njia za kidijitali. 

 

Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw Maharage Chande ameushukuru Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kulipatia Shirika la Posta vitendea kazi hivyo 250 ambavyo vitarahisisha shughuli za utendaji kazi ndani ya Shirika hilo. Ameeleza kuwa vifaa hivyo vitalisaidia Shirika kuongeza ufanisi wa kazi, utunzaji wa taarifa na kuhudumia wateja katika kasi inayoendana na dhana nzima ya "Posta Delivers Better".

Aliongeza kuwa Shirika liko kwenye mpango mkakati wa miezi 24 hadi 36 wenye kuhusisha mambo sita ambayo ni kuhakikisha wafanyakazi wana vitendea kazi vya kutosha na ujuzi wa kufanya kazi kidijitali, pili ni kuwaridhisha wateja wetu, kuongeza ufanisi na kasi ya kuhudumia jamii, mkakati wa kukuza mapato, Ubunifu wa kiteknolojia na mwisho ni mwonekano wa kisasa wa Shirika kwenye jamii inayoihudumia.

Imetolew na:
Kitengo cha Mawasiliano, 
Shirika la Posta Tanzania.

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA