JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

DPS ATEMBELEA BANDA LA POSTA SABASABA


Mkurugenzi wa Huduma za Posta wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Arubee Ngaruka, amepongeza ubunifu na maboresho ya muonekano wa Banda la Posta pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika hilo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).



Bw. Ngaruka ametoa pongezi hizo leo Julai 8, 2026, alipofanya ziara katika banda la Shirika la Posta huku akiambatana na viongozi wengine wa Shirika, ambapo alieleza kuridhishwa na namna banda hilo lilivyoboreshwa na jinsi huduma za Posta zinavyoendelea kuwafikia wananchi kwa ufanisi.



Aidha, katika ziara hiyo, Arubee amesifu uwepo wa idadi kubwa ya vyombo vya usafiri vya Posta vinavyotoa huduma ya usafirishaji wa wananchi ndani ya viwanja vya maonesho, akieleza kuwa huduma hiyo imeongeza urahisi wa usafiri kwa wageni wanaotembelea Sabasaba.



Meneja wa Banda la Posta Bw. Paul Mshanga, alimueleza Bw. Arubee kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika hilo pamoja na ubunifu unaotekelezwa na Posta kwenye maonesho hayo, ukiwa na lengo la kuwafikia wateja wengi zaidi na kuendelea kuboresha uzoefu wao wanapotembelea banda hilo.



Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za viongozi wa Shirika la Posta Tanzania za kufuatilia na kutathmini maendeleo ya ushiriki wa Shirika katika Maonesho ya Sabasaba, sambamba na kuhamasisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.



Imeandaliwa na;
Kitengo Cha Mawasiliano ,
Shirika la Posta Tanzania.


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA