JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

EMS YAFIKA KIGOMA KWA MKUU WA WILAYA


Uongozi wa Shirika la Posta Tanzania umetembelea ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Dkt. Rashid Chua Chua, kwa lengo la kumweleza kuhusu huduma ya usafirishaji wa vifurushi na bidhaa kwa njia ya haraka (Expedited Mail Service-EMS).

Ujumbe wa Shirika uliofika ofisini kwa Dkt. Chua Chua, uliongozwa na Bw. Arubee Ngaruka, Mkurugenzi wa Huduma za Posta, wengine ni Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika Bw. Ferdinand Kabyemela, Elia Madulesi, Lightness Mushi, Ahmad Rashid wa Posta Makao Makuu pamoja na Meneja wa Mkoa wa Kigoma Bw. Ndagije Chobaliko.

Akieleza makusudi ya ujio huo Bw. Kabyemela, amesema kuwa kupitia huduma ya EMS, wananchi na wafanyabiashara wa Kigoma wanaweza kusafirisha kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa urahisi bidhaa muhimu zinazopatikana katika Ziwa Tanganyika, ikiwemo samaki na dagaa, kwenda maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo Marekani na Canada.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Dkt. Rashid Chua Chua, amewapongeza viongozi hao kwa ujio wao mkoani Kigoma na kuwataka kuhakikisha huduma zinazotolewa zinawafikia wananchi kwa upana zaidi.

Mhe. Chua Chua amesisitiza umuhimu wa Shirika la Posta kutoa huduma zenye ubora na kuendelea kuzingatia mahitaji ya wananchi wa Kigoma, ili kuwawezesha kutumia fursa zilizopo katika usafirishaji wa bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Shirika la Posta Tanzania kuendelea kuhamasisha wananchi na wafanyabiashara kuhusu matumizi ya huduma za EMS, hasa katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka Kigoma kwenda maeneo mbalimbali duniani.

Imetolewa na
Kitengo Cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA