Habari
MHANDISI MAHUNDI AISIFU POSTA
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amelipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa jitihada zake za kuendelea kuboresha huduma zake kuwa za kidijitali huku likienda sambamba na maendeleo ya Teknolojia ya sasa.
Ameyasema hayo leo tarehe 19 Julai, 2024 wakati akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kutembelea Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo , katika Makao Makuu ya Posta jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika zaiara yake, Mhe. Naibu Waziri amelitaka Shirika la Posta Tanzania kutumia fursa ya maendeleo ya Teknolojia kuendelea kukuza Shirika kimapato na kuzidi kuongeza ubunifu ili huduma za Posta zizidi kukua kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Aidha Mhe. Mhandisi Mahundi amelipongeza Shirika kwa juhudi zake za kuboresha huduma ambazo zina unyumbufu wa kushirikiana na sekta binafsi kwa lengo la kuwahudumia wananchi kwenye maeneo mbalimbali kwa kutumia teknolojia mpya, akitolea mfano wa Ushirikiano aliouzindua kati ya Shirika na Azampesa mnamo tarehe 17 Julai, 2024 jijini Dar es Salaam.
Mhe. Naibu Waziri, Mhandisi Mahundi ameahidi kuendelea kushirikiana na Shirika la Posta na taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara yake ili kuhakikisha zinatoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi.
Kwa upande wake Postamasta Mkuu Bw. Maharage Chande wakati akitoa wasilisho lake ameeleza Mpango Mkakati wa Shirika wenye “Vikapu 6” ikiwemo Watu, Wateja, Kukuza Biashara, Teknolojia na Ubunifu, Ufanishi pamoja na Masoko vinavyolenga kuboresha utendaji sambamba na kuongeza mapato ya Shirika ili Shirika liendelee kuleta tija kwa Taifa.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania