Habari
HUDUMA PAMOJA YAJADILIWA NA WIZARA
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanya kikao maalumu na Shirika la Posta Tanzania kwa lengo la kujadili maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Huduma Pamoja unaotekelezwa na serikali kupitia Shirika la Posta Tanzania, ukiwa na dhamira ya kuboresha utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi.
Kikao hicho kimeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla. Pia walikuqepo viongozi mbalimbali wa Wizara na wadau wanaohusika na utekelezaji wa mradi huo, wakiwemo wakurugenzi kutoka wizara hiyo.
Vilevile, viongozi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora walishiriki kikao hicho kwa lengo la kujadili njia bora za kuimarisha utekelezaji wa mradi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Shirika la Posta Tanzania, Postamasta Mkuu, Macrice Mbodo, akiwa ndiye mtekelezaji na msimamizi wa mradi wa ukarabati wa vituo vya Huduma Pamoja na wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) wameshiriki katika kikao hicho.
Katika kikao hicho, washiriki walijadili maendeleo ya utekelezaji wa mradi, changamoto zinazojitokeza pamoja na mikakati ya kuhakikisha huduma za pamoja zinaboreshwa na kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Aidha, wakandarasi wanaofanya ukarabati wa vituo vya kutolea huduma wakamilishe ifikapo au kabla ya 30 Juni 2026. Wameaswa kuongeza kasi, ubunifu na usimamizi madhubuti wa kazi ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati uliopangwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
Imetolewa na;
Kitengo Cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

