JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

MBODO AHUDHURIA WARSHA YA UPU DRM


Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Bw. Macrice Mbodo, leo tarehe 25 Novemba 2024, amehudhuria ufunguzi rasmi wa warsha ya Umoja wa Posta Duniani (UPU) inayohusu Mpango wa kukabiliana na majanga (Disaster Risk Management) inayofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), jijini Arusha, Tanzania.
 
Warsha hiyo, ambayo itachukua siku tatu kuanzia tarehe 25 hadi 27 Novemba 2024, inahusisha wataalamu kutoka kanda ya Afrika wakiwa na uwakilishi kutoka nchi 45, ikiwa ni sehemu ya mpango wa msaada wa kiufundi wa UPU kupitia Idara ya Ushirikiano wa Maendeleo.
 
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Bw. Mbodo amesisitiza umuhimu wa maandalizi dhidi ya maafa na ustahimilivu, akitoa mfano wa uzoefu wa Tanzania, pamoja na mwitikio dhidi ya maporomoko ya ardhi ya Hanang yaliyotokea Desemba 2023. Ameeleza jinsi mifumo ya kukabiliana na majanga, ushirikiano wa serikali pamoja na UPU ulivyosaidia kuongeza ustahimilivu.
 
Pia, Bw. Mbodo amewaasa washiriki kutumia maarifa watakayopata katika warsha hii katika ngazi binafsi, mashirika na kitaifa, ili kuhakikisha uwepo kwa mifumo imara ya kukabiliana na majanga katika ukanda mzima wa Afrika.
 
Aidha, ameipongeza UPU na PAPU kwa misaada yao endelevu kupitia miradi kama hii ya mafunzo na kujenga uwezo. Pia amewakaribisha washiriki kufurahia uzuri wa asili na ukarimu wa jiji la Arusha.


 
Shirika la Posta Tanzania linawakilishwa na Zuhura Pinde (Mkuu wa Masuala ya Ndani), David Andrea (Mkuu wa Kitengo cha Ubora na vihatarishi ), Yusuph Mbwana (Afisa Mwandamizi wa Usalama), Gabriel Seleman (Afisa Upelelezi na Usalama), Ally Kipingu (Afisa Posta) na Monica Nkoba (Afisa Mwandamizi wa Rasilimali Watu).
 


 
Imeandaliwa na:
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA