JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

MKUTANO WA BARAZA LA UENDESHAJI LA UPU


Tanzania imeshiriki Mkutano wa Baraza la Uendeshaji la Umoja wa Posta Duniani (UPU) unaofanyika jijini Bern, nchini Uswisi, kuanzia tarehe 27 Aprili hadi 01 Mei 2026. Mkutano huu wa kawaida unajadili maendeleo ya utoaji wa huduma za posta duniani sambamba na mabadiliko makubwa ya kiuendeshaji katika sekta hiyo.

Mkutano huu ni wa pili kufanyika baada ya Mkutano Mkuu wa UPU uliofanyika mwezi Septemba 2025 jijini Dubai, ambapo ulipitishwa Mkakati wa miaka minne (2026–2029) wa kuendeleza huduma za posta. Mkakati huo unaweka misingi na mwelekeo wa utoaji wa huduma za posta katika kipindi hicho.

Katika mkutano huo, Baraza la Uendeshaji limepokea na kujadili taarifa kutoka katika Kamati zake tatu na kutoa mapendekezo yatakayowasilishwa katika Baraza la Utawala kwa ajili ya maamuzi ya utekelezaji.

Mkutano wa Baraza la Uendeshaji utafuatiwa na Mkutano wa Baraza la Utawala la UPU utakaofanyika kuanzia tarehe 04 hadi 08 Mei 2026. Baraza hilo litapokea mapendekezo yaliyotolewa ili kufanya maamuzi yatakayowezesha nchi wanachama kuanza utekelezaji kwa lengo la kuboresha huduma za posta duniani. Tanzania ni mjumbe wa mabaraza yote mawili ya Umoja wa Posta Duniani (UPU).

Ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Bi. Caroline Kanuti, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Posta kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Ujumbe huo pia unajumuisha Bwana Jasson Kalile kutoka Wizara hiyo, Bi. Clarence Ichwekeleza, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Ubora wa Huduma wa UPU akiwakilisha Kanda ya Afrika, Bwana Selemani Mwarabu, Mratibu wa Miradi ya UPU Taifa kutoka TPC, Abdullahaman Issa kutoka TCRA, pamoja na Pius Joseph, Constantine Kasese na Iddi Muhinda kutoka UCSAF, na ndugu Mashala Lufunga, Afisa Mkuu Mambo ya Posta Kimataifa kutoka TPC.

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano

Shirika la Posta Tanzania


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA