JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

MHE. KAIRUKI ATEMBELEA POSTA ZANZIBAR


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki(Mb), ametembelea Ofisi kuu ya Shirika la Posta  Kisiwani Unguja leo tarehe 26 Januari, 2026 kwa lengo la kujionea hali ya utoaji wa huduma za posta visiwani humo pamoja na maendeleo ya utekelezaji wa Mkakati wa Maboresho na Mageuzi ya Kidijitali katika sekta ya posta.

Katika ziara hiyo, Mhe. Kairuki aliongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohamed Abdullah pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Nicholaus Mkapa. Viongozi hao wamepokelewa na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo akiwa na Meneja Mkaazi Zanzibar Bi. Halima Abdulla pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Shirika la Posta. 

Mhe. Kairuki alipokea Wasilisho kutoka kwa Meneja Mkaazi Zanzibar Bi. Halima Abdullah pia alipata fursa ya kutembelea vitengo mbalimbali vya huduma, kusikiliza maelezo ya utendaji kazi, changamoto zilizopo pamoja na fursa za kuboresha huduma ili ziendane na mahitaji ya soko la kisasa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kairuki alisisitiza umuhimu wa Shirika la Posta kuendelea kubadilika na kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia na ushindani wa kibiashara, akieleza kuwa posta lazima ijiweke vizuri katika soko la ushindani kwa kubuni na kutoa huduma bunifu za kisasa na zenye kumlenga mteja.

_“Twende katika soko la ushindani na soko la kisasa. Posta ina nafasi kubwa sana ya kuchangia maendeleo ya uchumi wa kidijitali endapo itatumia kikamilifu teknolojia na rasilimali ilizonazo,” aliongea Mhe. Kairuki._

Wakati wa ziara hiyo, Waziri huyo aliipongeza Menejimenti ya Posta kwa juhudi zinazoendelea kufanywa katika kuimarisha huduma za kifedha, usafirishaji wa vifurushi, huduma za anwani za makazi na biashara pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usimamizi, ufanisi na ushindani wa taasisi zake ili ziendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la kisasa.

*Imetolewa na:*
*Kitengo cha Mawasiliano*
*Shirika la Posta Tanzania*


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA