JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

UFUNGUZI WA BARAZA LA WAFANYAKAZI


Dodoma

POSTA YATAKIWA KUBORESHA MSALAHI YA WAFANYAKAZI
 
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mha. Kundo Mathew amelitaka Shirika la Posta Tanzania Kuboresha maslahi ya wafanyakazi ili kuwaongezea morali wa kujituma katika utendaji wao.
 
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa 29 Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania tarehe 13 Januari, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Markdon, jijini Dodoma.
 
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mha. Kundo ambaye alimwakilisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari , Mhe Nape Nnauye amesisitiza kuwa uongozi wa Shirika hilo uboreshe mazingira ya utendaji kazi ikiwemo kuboresha vitendea kazi vitakavyowezesha kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi sambamba na mahitaji yao.
 
Aidha Naibu Waziri ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kuweka Sera, Sheria na Kanuni stahiki pamoja na kujenga na kuboresha miundombinu ya kitaifa ikiwemo, Anwani za Makazi na Postikodi, kuimarisha njia za usafirishaji huku lengo ikiwa ni kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa Shirika, ili kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kila siku ambayo kwa sasa yanabadilika kila kukicha. 
 
Mhe. Mha. Kundo ametumia nafasi hiyo kutoa wito wito kwa watendaji wa Shirika la Posta kuongeza juhudi na weledi katika utendaji wao ili kuongeza uzalishaji utakaoleta tija kwa Shirika na Taifa kwa ujumla.
 
Kwa upande wake Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo ameeleza kuwa mwelekeo wa Shirika ni kuifanya Posta kuwa ya kidijitali kupitia mpango mkakati wake wa nane (8) na hivyo kupitia kikao hiki watajadili mipango na mikakati ya kuwezesha utekelezaji wake.


*Imetolewa na;*
*Kitengo cha Mawasiliano*
*Shirika la Posta Tanzania*
*13 Januari, 2023*

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA