Habari
PMG AFANYA KIKAO NA WAFANYAKAZI
▪️ Shirika lavuka malengo ya mapato na faida
▪️ Wafanyakazi na mikoa iliyofanya vizuri watambuliwa
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo, amefanya kikao na wafanyakazi wa Shirika kwa ajili ya kutoa mrejesho wa utendaji wa Shirika kwa kipindi cha Robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2025/26, leo tarehe 29 Mei, 2026 katika ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza.
Kikao hicho kimehusisha wafanyakazi kutoka Makao Makuu, Zanzibar, pamoja na mikoa yote nchini, ambapo Postamasta Mkuu aliwasilisha taarifa ya mafanikio ya Shirika katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026, mafanikio yaliyopatikana katika uzalishaji wa mapato na faida, ubora wa huduma pamoja na vipaumbele vya Shirika kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mbodo amewapongeza wafanyakazi kwa juhudi kubwa zinazochangia kuendelea kuimarika kwa utendaji wa Shirika na kusisitiza umuhimu wa kuongeza ubunifu, uwajibikaji na ushirikiano katika kuhakikisha Shirika linaendelea kufikia malengo yake ya biashara na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, ametambua na kuipongeza mikoa iliyofanya vizuri katika uzalishaji wa mapato. Pia amewapongeza watumishi waliopata tuzo mbalimbali, walioteuliwa katika nafasi za uongozi, pamoja na wafanyakazi kutoka mikoa iliyofanya vizuri watakaoshiriki ziara za mafunzo katika mikoa mbalimbali nchini kama sehemu ya kuhamasisha utendaji bora na kujifunza zaidi.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeendelea kuonesha dhamira ya Shirika la Posta Tanzania ya kujenga taasisi ya kisasa, yenye ushindani, inayotoa huduma bora na inayochangia kikamilifu maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Imeandaliwa na:
Kitengo Cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.

