Habari
POSTA IWENI NA UONGOZI WA KIMKAKATI
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb), ameelekeza Shirika la Posta Tanzania kuwa na uongozi wa kimkakati na kila mfanyakazi awajibike ipasavyo ili Shirika lijiendeshe kwa ubunifu na kibiashara.
Ametoa wito huo, wakati alipofanya ziara yake ya kikazi katika Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania leo tarehe 27 Novemba, 2025 jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Kairuki ameongeza kuwa Posta inapaswa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha huduma za Posta na kuongeza uwekezaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuchambua vyanzo vya mapato, ili kuimarisha vinavyoleta tija na kuboresha vyanzo visivyochangia mapato ya kutosha.
Mhe. Waziri pia ameelekeza Posta kufanya mchakato wa uchambuzi wa viashiria vya hatari (risk analysis) ili kuimarisha mifumo ya usalama, na kufanyia mapitio mifumo kila baada ya miezi sita ili kulinda taarifa na mizigo ya wateja.
Katika hatua nyingine Mhe. Angellah Kairuki ameipongeza Posta kwa ubunifu wake ikiwemo uanzishwaji wa duka mtandao (Kiepeo Shop) huku akihimiza juhudi zaidi za kutafuta wateja na kuimarisha uaminifu wa mfumo huo. Pia ameagiza kuwe na mabalozi wa huduma za Posta wenye taswira chanya ili kuongeza uelewa wa huduma za Posta.
Vilevile Waziri Kairuki ameahidi ushirikiano katika mageuzi ya kidigitali na kuhakikisha Posta inakuwa taasisi ya kisasa kwa maendeleo ya Taifa.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb), alipotembelea ofisi za Posta kuu jijini Dar es Salaam huku akiwa ameambatana na Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo, viongozi wa Wizara pamoja na uongozi wa Shirika la Posta Tanzania, kwa ajili ya kujionea shughuli za utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania

