Habari
POSTA KUSHIRIKIANA NA TANTRADE

Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) wametiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara kwa ajili ya Maonesho ya 49 (SABASABA 2025), yatakayofanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2025 katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Kupitia makubaliano haya, Posta itatoa huduma zifuatazo:
* Usafirishaji wa mizigo, bidhaa na vifaa vya maonesho kutoka au kwenda kwenye mabanda ya washiriki.
* Usafiri wa wageni maalum (VIPs) kuzunguka viwanja vya SABASABA kwa usafiri wa uhakika.
* Huduma ya SWIFPACK, inayoruhusu mteja kuomba usafirishaji wa mizigo moja kwa moja kupitia simu janja.
* Huduma ya Cargo & Clearing kwa washiriki wa kimataifa wanaoleta bidhaa kutoka nje ya nchi.
* Duka la mtandaoni la Posta, ambapo bidhaa za washiriki zitapatikana kwa wanunuzi duniani kote.
Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bi. Latifa M. Khamis, alieleza kuwa ushirikiano huu utarahisisha uendeshaji wa maonesho na kuongeza mvuto wa SABASABA 2025 kwa wadau wa ndani na wa nje ya nchi.
Kwa mara ya kwanza, wananchi wataweza kununua bidhaa kutoka kwenye maonesho na kuzifikisha maeneo mbalimbali kulingana na matakwa yao kupitia Posta, huku washiriki wa kimataifa wakihakikishiwa usalama na ufanisi wa mizigo yao kutoka nchi zao hadi katika viwanja vya SABASABA.
Imeandaliwa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania