JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

POSTA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA NIDA


Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Bw. Maharage Chande amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mhandisi Ismail Rumatila tarehe 10 Mei, 2024 Katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalilenga kuboresha ushirikiano katika utekelezaji wa mradi wa Huduma Pamoja yaani kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kiserikali zinafika karibu zaidi na wananchi kupitia mifumo ya NIDA, mazungumzo hayo yamefanyika ikiwa ni mwendelezo wa makubaliano ya Ushirikiano wa Kibiashara (MoU) baina ya TPC na NIDA ambayo yalishafanyika hapo awali.

Utekelezaji wa mradi huu wa Huduma Pamoja ulianza na mfumo wa one roof lakini sasa unaendelea kutekelezwa lengo ikiwa ni kutumia mfumo wa single window (dirisha moja) ambapo taarifa za anayepatiwa huduma (mfano alama za vidole, picha n.k) zitawekwa kwenye mfumo (portal ) na kutumwa kwa watendaji wa taasisi husika kwa ajili ya kuzifanyia kazi na kurejeshwa baada ya kukamilika ili kumfikia mteja.

Bw. Maharage alisisitiza kwamba utekelezaji wa hili unagusa mabadiliko katika michakato ya kiutendaji (business process) na hivyo kuchagiza upatikanaji wa huduma bora kwa haraka.

Mazungumzo hayo yaligusia pia suala la ushirikiano katika kusambaza vitambulisho vya taifa ambavyo havijawafikia walengwa kupitia NIDA, ambapo POSTA iko tayari kusambaza vitambulisho hivyo.

Vilevile, Bw. Maharage alielezea namna huduma za Posta zilivyoboreshwa na kuwa Posta ipo tayari kuwasafirishia kontena, mizigo mikubwa yoyote (cargo), vifurushi na barua popote pale ndani na nje ya nchi.

Bw. Maharage aliongeza kuwa Posta imepata leseni ya clearing and forwarding hivyo kwa sasa ina mashirikiano na TRA – upande wa forodha ambapo mzigo ukipokelewa unafanyiwa clearing na kuweza kukufikishia mahali ulipo bila usumbufu wa kutakiwa kufika POSTA kwa ajili ya taratibu za forodha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA amekubali na kuridhia ushirikiano huo na amewaagiza wataalamu wake kukutana mara moja na wataalamu wa TPC kwa lengo la kuweka sawa mifumo ya kiutendaji ili kufanikisha utekelezaji wa makubaliano hayo.

Postamasta Mkuu Bw. Maharage Chande aliambatana na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Serikali wa TPC Bi. Aicha Nangawe.

 

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano

Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA