JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

POSTA TANZANIA YAGUSA JAMII


Shirika la Posta Tanzania linaendelea kutekeleza wajibu wake kwa jamii kwa kutoa huduma ya bure ya upimaji wa afya (Afya Check) kwa wakazi wa Buguruni na maeneo jirani. Huduma hii ilihusisha upimaji wa kisukari, presha ya damu, saratani ya mlango wa kizazi, tezi dume na vipimo vingine muhimu.  

Katika kuendeleza mchango kwa jamii, Shirika pia limekabidhi vifaa tiba na mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusaidia na kuleta faraja kwa wahitaji.  

Akizungumza kwa niaba ya Postamasta Mkuu, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo Bw. Ferdinand Kabyemela alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya kuthamini mchango wa jamii katika mafanikio ya Shirika na kuonesha uwajibikaji wa kijamii.  

Aidha, alisisitiza  na kuwahamasisha wananchi kuhuisha taarifa zao pamoja na kulipia Ada ya Masanduku vilevile waendelee kutumia huduma za kisasa na kidijitali kama Duka Mtandao, Posta Kiganjani na Swifpack kwa ajili ya biashara, usafirishaji na malipo kwa njia rahisi na salama.

Kwa upande wake Dkt Haki Paul Mhozya, Mratibu wa Tiba na Muwezeshaji wa magonjwa yasiyoambukiza (NCD)kutoka kituo cha Afya Buguruni, amelipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa kugusa maisha ya wananchi na kutoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano wa Shirika ili kuhudumia jamii ambayo ina mahitaji makubwa ya afya, pia ameitaka jamii kuwa makini na maradhi yasiyoambukiza kwa kujitokeza kupima ili kujua hali zao. 

Mwakilishi wa Postamasta Mkuu Bw. Kabyemela aliambatana  na Bw. Elia Madulesi (Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mambo ya Posta Kimataifa), Bw. Michael Mwanachuo (Meneja Masoko) pamoja na maafisa wengine waandamizi kutoka Posta. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA