Habari
POSTA YATWAA TUZO YA MSHINDI WA KWANZA

Shirika la Posta Tanzania limeibuka kidedea kwa kutwaa Tuzo ya Mshindi wa Kwanza katika kipengele cha Watoa Huduma za Usafirishaji na Usafiri kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA 2025).
Tuzo hiyo imekabidhiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), na kupokelewa kwa heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania Balozi Meja Jenerali (Mstaafu) Gaudence Salim Milanzi, katika hafla ya kilele cha maonesho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa.
Ushindi huu umetokana na ubunifu mkubwa ulioonyeshwa na Shirika katika utoaji wa huduma zake, ikiwemo huduma ya kipekee ya Royal Buggies (usafiri wa umeme kwa wageni ndani ya viwanja), huduma za kisasa za PostCargo, pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali kama SwifPack, Posta Kiganjani, na Duka Mtandao.
Tuzo hii ni kielelezo cha dhamira ya Shirika la Posta ya kuendelea kuwa suluhisho la kisasa la usafirishaji na mawasiliano kwa Watanzania, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhimiza mageuzi ya kidijitali na uchumi wa viwanda.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania