Habari
POSTAMASTA MKUU AFUNGUA KIKAO
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo, amefungua rasmi Kikao cha 42 cha Baraza la Majadiliano kilichofanyika Mei 20, 2026 katika Hoteli ya PH EXECUTIVE, mjini Morogoro, huku akisisitiza umuhimu wa mageuzi ya kidijitali, uwajibikaji na ushirikiano katika kufanikisha malengo ya kimkakati ya Shirika.
Katika hotuba yake, Bw. Mbodo amewashukuru viongozi na wajumbe wote wa Baraza la Majadiliano, akiwemo Mwenyekiti Ndugu Mabruki Makame pamoja na Kamishna Junus Ndaro, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TEWUTA, kwa kuhudhuria kikao hicho muhimu.
Akizungumzia ajenda za kikao hicho, Bw. Mbodo, amesema kuwa zitahusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tisa, kuingiza mipango ya kazi katika mfumo wa PEPMIS, pamoja na hoja mbalimbali za wafanyakazi.
Kwa mujibu wa Postamasta Mkuu, Mpango Mkakati wa Tisa (2026–2030) unalenga kuifanya Posta Tanzania kuwa mtandao wa posta wa kidijitali unaoaminika zaidi nchini, ukiunganisha wananchi, serikali na biashara kupitia huduma bora, ubunifu na teknolojia ya kisasa. Mpango huo umejengwa katika nguzo sita; watu, maadili na Uongozi, mageuzi ya kidijitali, ubora wa huduma, ukuaji wa biashara, ushirikiano na uendelevu.
Aidha, ameeleza kuwa Shirika la Posta Tanzania linakusudia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote, kurejesha Chuo cha Posta kwa mfumo wa kidijitali ambacho pia kitatoa mafunzo Kwa nchi za jirani na hivyo kuongeza mapato Kwa Shirika, kuboresha vifaa vya kisasa katika ofisi zote, pamoja na kuimarisha mafunzo na programu za kuwajengea uwezo watumishi.
Katika hitimisho, Bw. Mbodo amewataka wajumbe wa Baraza kushiriki majadiliano kwa uwazi, weledi na mshikamano ili kuhakikisha mafanikio ya Mpango Mkakati wa Tisa yanapatikana kwa manufaa ya Shirika na Taifa kwa ujumla.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

