JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

MAADHIMISHO YA SIKU YA POSTA AFRIKA


Dodoma
18 Januari, 2022  

POSTA  KUBADILI AFRIKA KUWA YA KIDIJITI

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye ameelezea namna ambavyo Tanzania ina imani na Shirika la Posta Tanzania kupitia huduma linazozitoa kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Posta Barani Afrika  yatawezesha kuibadili Afrika kuwa ya kidijitali kama ilivyokusudiwa katika Azimio la Umoja wa Afrika (AU) kwa (2020-2030).
 
Ameeleza hayo wakati alipokuwa akihitimisha kilele cha Maadhimisho ya miaka 43 ya Umoja wa Posta Afrika yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 18 Januari, 2023, katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF, jijini Dodoma.
 
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Nape amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itahakikisha huduma za Posta nchini zinazidi kuboreshwa na kukua ili kuendana na mapinduzi ya teknolojia Duniani ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Posta kuwafikia wananchi wote Barani Afrika.
 
Katika hatua nyingine, Mhe. Nape ameongeza kuwa, Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa   Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuongeza juhudi katika kukamilisha ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja huo (PAPU) yaliyopo jijini Arusha, ambapo jengo hilo litakapokamilika, na kuanza kutumika litaongeza ufanisi wa Umoja huo katika kutoa huduma na pia litazalisha ajira zaidi kwa Watanzania.  
 
Naye Naibu katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdullah kwa niaba ya katibu Mkuu Wizara hiyo ameupongeza Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kwa kuendelea kuunga mkono juhuzi za Sekta ya Posta Barani Afrika hususan katika huduma za kimtandao lengo likiwa kurahsisha huduma za Posta kwa wananchi.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mtendaji wa umoja wa Posta Afrika, Dkt. Sifundo Chief Moyo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuweka mazingira wezeshi husan uwekaji wa Mundombinu wa Anuani za makazi na Postikodi inayowezesha watoa huduma za Posta kuwafikia wananchi mahali popote walipo kwaurahisi zaidi.
 
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Bakari ameeleza kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta ya Posta nchini hususani katika maendeleo ya teknolojia yanayoendelea sasa duniani yanayohamasisha uwepo wa huduma mtandao zinazorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, TCRA iko tayari kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa changamoto zozote zitakazojitokeza katika kuwezesha huduma mtandao hasa katika mipakani mwa nchi yetu
 
Aidha, Meneja wa Posta Mkoa wa Dodoma Bw. Ferdinand Kabyemela kwa niaba ya Postamasta Mkuu ameeleza kuwa Posta itaendelea kuwa mwezeshaji mahiri wa biashara zote za kuvuka mipaka na za mtandaoni (e-commerce) na zisizo za mtandaoni kwani miundombinu ipo, uwezo na ujuzi upo, nia thabiti pia ipo katika kuwezesha huduma za biashara mtandao zinazovuka mipaka na zisizovuka mipaka.
 
 *Imetolewa na;*
*Kitengo cha Mawasiliano,*
*Shirika la Posta Tanzania*
*18 Januari, 2023*

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA