Habari
SEKTA YA POSTA KUBUNI MBINU BUNIFU

Tanzania kupitia Shirika la Posta Tanzania imejipanga kuendelea kubuni mbinu bunifu katika utoaji wa huduma zake ili kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na huduma za Posta ndani na nje ya nchi.
Hayo yameelezwa tarehe 23 Juni, 2025, katika ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) jijini Arusha na Bw. Deogratius Kwiyukwa kwa niaba ya Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo wakati akishiriki mjadala uliohusisha Wakurugenzi Wakuu wa Sekta ya Posta na kujadili namna ambavyo nchi wanachama PAPU na mashirika ya Posta itakavyotafuta suluhisho na Fursa za Ufadhili wa Huduma za msingi za Posta.
Bw. Kwiyukwa alieleza kuwa Sekta ya Posta inakabiliwa na changamoto kubwa ya kugharamia utoaji wa huduma za Posta kwa wote, hususan katika maeneo yenye changamoto za kijiografia au zenye idadi ndogo ya watu na ili kudumisha na kuboresha huduma hizi, ni muhimu kubuni vyanzo vipya vya ufadhili na kutumia mbinu bunifu zinazolenga kuboresha ufanisi na uendelevu wa kifedha.
Aidha, majadiliano haya yalichambua mikakati mbalimbali kama vile ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, uanzishwaji wa mifuko ya huduma kwa wote, na kubadilisha wigo wa huduma za posta kuendana na wakati. Pia kuangalia nafasi ya usimamizi bora wa gharama, uwazi, na ushirikiano wa kikanda chini ya usimamizi wa PAPU, kuhakikisha kwamba huduma za Posta zinaendelea kuwafikia wananchi wote kwa bei nafuu na kwa ufanisi.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania