JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

SERIKALI YAKABIDHI MAGARI 12 KWA TPC


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb) kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba(Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekabidhi  magari 12 yenye themani ya Shs.2.2 bilioni kwa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake ya kuwahudumia wananchi wa Tanzania.
                   

Mhe. Kairuki amekabidhi magari kwa Postamasta Mkuu na kwa Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kutumika na Shirika la Posta upande wa Zanzibar.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 8 Februari, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JNICC), wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi ambapo yameshudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo Balozi Meja Jenerali (Mstaafu) Gaudence Milanzi.

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo amesema Shirika liliandaa na kuwasilisha Serikalini maombi ya Mradi uliobainisha mahitaji ya usafiri kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake. " Serikali baada ya kuyapitia na kuyahakiki wameweza kutupatia Magari haya ikiwa na lengo la kuboresha utoaji wa huduma zetu".
 
Bw. Mbodo amefafanua kuwa Shirika limepata magari sita ya Tani 3.5, magari manne ya Tani 10, pamoja na Trailer na kichwa kimoja kitakachotumika kuvuta trailer hiyo ambayo itatumika katika usafirishaji wa mizigo, vifurushi na huduma nyingine za kibiashara katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika hatua nyingine Bw. Mbodo ameeleza kuwa, Shirika hili limefanikiwa kujipambanua vema kwa kutumia rasilimali zake za ndani kwa kununua bajaji 40  zenye thamani ya Shilingi million 200 zinazotumia nishati ya Umeme zinazokwenda kutumika kutoa huduma za haraka, hususan za kufikisha vifurushi, nyaraka na bidhaa kwa wateja katika maeneo ya mijini na yenye msongamano.

Aidha, Bw. Mbodo amesema kuwa, upatikanaji wa magari na bajaji hizo utaongeza ufanisi wa kiutendaji, kupanua wigo wa huduma za kibiashara na kuboresha uzoefu wa wateja. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA