Habari
SHIRIKA LA POSTA LANG’ARA KWENYE TUZO
Shirika la Posta Tanzania limeibuka mshindi wa Tuzo ya Ubunifu wa Sekta ya Umma, ijulikanayo kama "Digital Transformation Award 2025" (TPSIA), ikiwa ni kutambua mchango wa mkubwa wa Shirika hilo katika mabadiliko ya kidijiti na uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Tuzo hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Sharf. A. Sharif katika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam, ambapo Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Ferdinand Kabyemela kwa niaba ya Postamasta Mkuu alipokea tuzo hiyo.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo Bw. Kabyemela alieleza kuwa ushindi huo ni ushahidi wa wazi wa dhamira ya dhati ya Posta katika kuleta mageuzi ya kidijitali na kuimarisha huduma za Posta na usafirishaji nchini.
Ushindi wa tuzo hiyo umetokana na tathmini ya vigezo mbalimbali ikiwemo ubora wa huduma, ubunifu, matokeo ya utendaji, uwajibikaji, uongozi bora, ushirikishwaji wa wadau na uendelevu wa mifumo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.

