JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

SWIFPACK CHACHU YA MAFANIKIO


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa ameagiza Shirika la Posta Tanzania kuimarisha ufuatiliaji na ubora wa huduma ya SWIFPACK ili kuepuka ucheleweshaji wa huduma usafirishaji na kujenga imani kwa wateja.

Ameeleza hayo wakati wa uzinduzi wa huduma mpya ya Shirika la Posta ijulikanayo kwa jina la SWIFPACK, leo tarehe 24 Januari, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Onomo jijini Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Waziri Silaa amelitaka Shirika la Posta Tanzania  kuweka mifumo thabiti ya kusimamia madereva katika maadili kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi pamoja na watoa huduma wengine  ili kukidhi mahitaji ya wateja na urahisi wa huduma.

Aidha, Waziri Silaa amelipongeza Shirika la Posta kwa kuwa na ubunifu wa kuleta huduma mpya ya SWIFPACK huku akilitaka Shirika kuwa chachu na kufungua milango ya mafanikio makubwa kwa Shirika, wananchi, madereva wa bodaboda, bajaji na magari binafsi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa amemshukuru Waziri Silaa kwa kuwa karibu na Taasisi zake ili kuchochea ubunifu katika kipindi hiki ambacho teknolojia inachukua kasi kubwa ya kushughulikia masuala mbalimbali ya maisha ya wananchi kwa dunia nzima.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Tanzania Balozi Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Salim Milanzi, ametumia nafasi hiyo kuahidi kutekeleza maagizo kwa  weledi ili huduma ya SWIFPACK iweze kuwa suluhisho bora kwa wananchi.

Naye, Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo amesema kuwa huduma hii ya SWIFPACK inakwenda kuwarahisishia wananchi huduma ya usafirishaji wa vifurushi, mizigo na abiria sambamba na kuongeza ajira kwa vijana wa bodaboda, bajaji na magari binafsi.

SWIFPACK ni huduma inayopatikana kwa kupakua aplikesheni yake ndani ya PlayStore na Appstore huku ikijumuisha usafirishaji wa mizigo midogo na mikubwa inayoweza kufika hadi tani 30, pia usafirishaji wa abiria mijini na vijijini na ni mfumo wa kiteknolojia unaomuwezesha mteja kufuatlia mzigo wake muda wote.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano

Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA