JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

SWIFPACK KWA WAFANYABIASHARA


Shirika la Posta Tanzania (TPC) limeshiriki Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo uliofanyika tarehe 25 Aprili 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo lilitumia jukwaa hilo kuwasilisha fursa mbalimbali za huduma zinazolenga kurahisisha biashara na kuongeza ufanisi kwa wafanyabiashara.

Akizungumza katika mkutano huo, Meneja wa Posta, Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Mshanga, aliwahimiza wafanyabiashara kuchangamkia huduma zinazotolewa na Shirika la Posta, hususani huduma za SwifPack, PostCargo pamoja na duka mtandao la Posta (Kipepeo Shop), zinazosaidia kurahisisha usafirishaji wa mizigo na upatikanaji wa masoko ya bidhaa.

Bw. Mshanga, alieleza kuwa huduma ya SwifPack inawawezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa ndani ya nchi kwa haraka na kufuatilia mizigo yao kwa wakati halisi. Aidha, alibainisha kuwa PostCargo inalenga usafirishaji wa mizigo mikubwa na ya kibiashara kwa gharama nafuu, huku Kipepeo Shop likiwa jukwaa la kidijitali linalowaunganisha wafanyabiashara na wateja kwa urahisi zaidi kupitia mauzo ya mtandaoni.

Alisisitiza kuwa mfanyabiashara wa leo anahitaji suluhisho jumuishi linalounganisha usafirishaji na masoko ya bidhaa, na kwamba huduma hizi zimeboreshwa mahsusi kukidhi mahitaji hayo.

Vilevile, timu ya masoko na mauzo ya Shirika la Posta ilifanya mazungumzo ya ana kwa ana na wafanyabiashara mbalimbali, ikitoa maelezo ya kina kuhusu fursa zilizopo na namna ya kunufaika na huduma hizo kulingana na mahitaji ya kila mfanyabiashara.

Aidha, alibainisha kuwa Shirika la Posta linaendelea kuboresha huduma zake ili ziendane na mabadiliko ya kidijitali na mahitaji ya soko, ikiwa ni pamoja na huduma za kifedha na usambazaji zinazolenga kurahisisha shughuli za kibiashara.


Mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa biashara na taasisi, ukiwa na lengo la kujadili maendeleo ya biashara, changamoto zinazowakabili wafanyabiashara pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Ushiriki wa Shirika la Posta Tanzania, umeendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi na sekta binafsi, huku ukiwapa wafanyabiashara uelewa mpana wa fursa zilizopo katika huduma za usafirishaji, kidijitali na masoko ya mtandaoni.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA