JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

POSTA TANZANIA KIMATAIFA


Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Maharage Chande amefanya mazungumzo ya kushirikiana kibiashara na mashirika ya Posta makubwa duniani ili kuhakikisha bidhaa (Barua,vipeto,vifurushi na Mizigo) zinazotumwa kutoka mataifa hayo kuja Tanzania zinapitia Shirika la Posta.

Hayo yamebainika baada ya Bwana Maharage kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Posta za Marekani, Uchina, Uingereza, Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E-Dubai) na Oman wakati wa vikao vya Baraza la Utawala la  Umoja wa Posta Duniani (UPU) lililokuwa linaendelea kuanzia 29 April hadi 3 Mei, 2024 jijini Berne, nchini Uswiss yalipo Makao Makuu ya Umoja wa Posta Duniani.

Mbali na vikao hivyo, pia Postamasta Mkuu amefanya mazungumzo na makampuni makubwa yanayojihusika na biashara mtandao yakiwemo China Express Association yenye makao makuu yake jijini Beijing, SF Express yenye Makao makuu jijini Shenzhen, Uchina na CAINIAO  ya jijini Beijing, China.

Vikao hivyo vimekuwa na mwitiko mkubwa kutoka mataifa hayo na makampuni hayo ambayo yamepongeza mageuzi yanayofanywa na Posta ya Tanzania chini ya Kaulimbiu ya Posta Tunafikisha Vizuri (Posta Delivers Better) vimefanyika pembeni mwa vikao vya Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Duniani vinavyoendelea jijini Berne, Uswis.

Postamasta Mkuu Bw. Maharage Chande yupo nchini Uswis kushiriki vikao vya Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Duniani akiongozana na Bw. Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Wengine walioongozana na Postamasta Mkuu katika mazunguzo hayo ni Bw. Constantine Kasese, Mkurugenzi wa Biashara Mtandao na Huduma za Fedha (Shirika la Posta), Bw. Elia Madulesi Meneja Uhusiano (Shirika la Posta).

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano

Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA