Habari
TANZANIA YASHIRIKI MAJADILIANO
Arusha
29 Novemba, 2024
*TANZANIA YASHIRIKI JUKWAA LA MAJADILIANO NAMNA YA KUKOKOTOA MALIPO/TOZO ZA BIDHAA ZA POSTA KIMATAIFA*
Shirika la Posta Tanzania limeshiriki ufunguzi wa Jukwaa liliyoandaliwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) kwa kushirikiana na Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kwa ajili ya ukokotoaji wa tozo za kuhudumia barua , vipeto na vifurushi vinavyopitia mfumo wa posta kwa nchi wananchama wa UPU.
Akizungumza kwa niaba ya Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), wakati wa ufunguzi uliofanyika tarehe 28 Novemba, 2024 katika makao makuu ya PAPU jijini Arusha Bw. Elia Madulesi, Mkuu wa Mawasiliano na Masuala ya Posta Kimataifa, aliwakaribisha wataalamu hao kutoka nchi zote barani Afrika wanaohudhuria jukwaa hilo jijini Arusha.
Bw. Madulesi alizungumzia dhamira ya TPC kuimarisha shughuli zake kupitia mabadiliko ya kidigitali, kupanua huduma za barua na kuboresha uwezo wa usafirishaji ili kuendana na ukuaji wa sekta ya biashara mtandao (e-commerce) inayokua kwa kasi duniani kote.
Aidha, Bw. Madulesi alibainisha kuwa ili kuendeleza juhudi hizi, TPC inategemea kwa kiasi kikubwa mfumo wa kulipana wa kimataifa ulio wa haki, ambao una jukumu muhimu katika kuhakikisha ubunifu na ukuaji wa huduma za posta duniani kote.
Katika hatua nyingine, Bw. Madulesi alitumia fursa hiyo kuwahimiza wataalamu hao kuzingatia yanayojadiliwa kwenye jukwaa hilo, hasa kuhusu mapendekezo ya vikokotoo vitakavyowasilishwa kwenye Mabaraza UPU na baadae kwenye Mkutano Mkuu wa UPU mwezi Septemba 2025 huko Dubai kwa ajili ya maamuzi ya mwisho kutoka kwa mawaziri wenye dhamana ya Posta.
Jukwaa hilo la siku mbili kuazia tarehe 28 -29 Novemba, 2024 limeendeshwa na wataalamu watano kutoka UPU ambao walipitia maeneo mbalimbali yanayoratajiwa kufanyiwa mabadiliko kwenye msimu ujao wa Mkakati wa Posta wa Dunia (2026-2029).
*Imeandaliwa na:*
*Kitengo cha Mawasiliano*
*Shirika la Posta Tanzania*