Habari
TPC NA DCEA TUMEJIPANGA
Shirika la Posta Tanzania limeingia makubaliano ya ushirikiano kati yake na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), lengo likiwa ni kudhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia mifumo ya usafirishaji wa mizigo ya Shirika. Tukio hili limefanyika leo tarehe 19 Disemba 2024 katika ofisi za DCEA jijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na viongozi waandamizi wa pande zote mbili.
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo, amesema kuwa makubaliano haya ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa huduma za Posta na kuhakikisha kuwa Shirika linakuwa njia salama ya usafirishaji wa mizigo kwa Watanzania. "Kupitia ushirikiano huu, tumejidhatiti kuimarisha mifumo yetu ya usalama kwa kutumia mashine za kisasa za kubaini dawa za kulevya na kuweka afisa maalum anayesimamia ukaguzi wa mizigo kwa ukaribu," alisema Bw. Mbodo.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Bw. Aretas Lyimo, amepongeza hatua hii ya Shirika la Posta Tanzania na kusisitiza kuwa ushirikiano huu utasaidia kufanikisha jitihada za Serikali za kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, ambayo imekuwa ikileta athari kubwa kwa jamii na uchumi wa nchi. Amesema, “Ushirikiano huu ni mwanzo mpya wa kuimarisha mifumo ya udhibiti ili kuhakikisha kwamba vifurushi vyote vinavyoingia na kutoka nchini vinakaguliwa ili kuhakikisha kwamba hakuna usafirishaji wowote wa dawa za kulevya zinazoweza kutoka nje ya mipaka yetu au kuingia ndani ya mipaka yetu.”
Makubaliano haya yanajumuisha kuweka mfumo wa kubadilishana taarifa za kiusalama, kutoa mafunzo kwa watendaji wa pande zote, na kutumia vifaa vya kisasa katika ukaguzi wa mizigo. Viongozi wa taasisi zote wameeleza dhamira yao ya kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti uhalifu na kulinda usalama wa Taifa.
Shirika la Posta limeahidi kushirikiana kwa dhati na DCEA katika kutekeleza vipengele vya makubaliano haya, ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na kuhakikisha kuwa linabaki kuwa chombo kinachoaminika katika utoaji wa huduma za posta.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania