Habari
POSTA YAPATA MAFUNZO,
Dodoma
28 Novemba, 2023
SHIRIKA LA POSTA LAPATA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA MAAFA.
Mafunzo ya siku nne ya kukabiliana na Maafa yanayoratibiwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU), Ofisi ya Waziri Mkuu, na Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika la Posta yameanza leo Jijini Dodoma.
Mafunzo hayo yanatolewa ili kuwajengea uwezo na ujuzi watendaji na viongozi kutoka Kitengo cha Mambo ya Ndani, Kitengo cha Udhibiti wa Vihatarishi na Ubora pamoja na wawakilishi wa baadhi ya Mikoa pamoja na Zanzibar, ili waweze kupata uelewa wa Sheria ya Maafa 2015 na kanuni zake za mwaka 2017, waweze kujiandaa na kukabiliana na Maafa, kufanya tathmini ya Mahitaji Baada ya Maafa (PDNA) ndani ya Shirika, pamoja na kuratibu na kufuatilia, usimamizi na tathmini ya ndani ya kukabiliana na Maafa.
Mafunzo hayo yanatolewa na Mkufunzi Mshauri Elekezi (Consultant) kutoka Umoja wa Posta Duniani, Bi. Vivaoliva Shoo ambaye ameeleza mambo kadhaa ikiwemo namna ya kugundua vihatarishi mahala pa kazi, namna ya kujiandaa na kukabiliana na majanga katika maeneo ya utendaji ndani na nje ya Shirika.
Aidha Bi. Vivaoliva alishauri kuwa, kutokana na ukubwa na unyeti wa shughuli zinazofanywa na Shirika la Posta, linatakiwa kushiriki na kuhusika moja kwa moja katika Kamati ya Kitaifa ya Maafa inayoongozwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ili iweze kuhusika katika upangaji wa mikakati ya kuzuia maafa katika shughuli za usafirishaji nchini.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika la Posta, Bi. Zuhura Pinde amewataka washiriki hao kuzingatia mafunzo hayo ili yaweze kuleta tija kwa Shirika na kuzuia majanga mbalimbali yanayoweza kuleta hasara ndani ya Shirika.
Mafunzo hayo yanahudhuriwa na ujumbe kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa, ujumbe kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Masoko na Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania.
Mkufunzi Mshauri Elekezi (Consultant) kutoka Umoja wa Posta Duniani, Bi. Vivaoliva Shoo akitoa mafunzo ya kukabiliana na maafa. Mafunzo hayo yanaratibiwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU), Ofisi ya Waziri Mkuu, na Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika la Posta.
Mkuu wa Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika la Posta, Bi. Zuhura Pinde akizungumza wakati wa Mafunzo ya kukabiliana na maafa yanayoratibiwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU), Ofisi ya Waziri Mkuu, na Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika la Posta.
Meneja wa Posta Mkoa wa Dodoma, Bw. James Dongwe akizungumza wakati wa mafunzo hayo.