JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

POSTA NA AZAMPESA KULETA SULUHISHO


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amewaasa Shirika la Posta Tanzania pamoja na AzamPesa kuhakikisha wanaleta suluhisho la malipo ya kisasa ya fedha utakaowawezesha wananchi kulipia huduma mbalimbali za kijamii kupitia simu zao za mkononi.
 
Hayo ameyasema leo tarehe 17 Julai, 2024 kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye wakati akizindua ushirikiano wa kibiashara kati ya Shirika la Posta Tanzania na AzamPesa, jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mhandisi Mahundi ameeleza kuwa ushirikiano huu utaongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi, hususan wale waishio vijijini ambako huduma hizi hazipatikani kwa urahisi sambamba na kutoa fursa kwa ofisi za Posta zaidi ya 300 nchini kuwa na uwezo wa kutoa huduma za kifedha za AzamPesa.
 
Aidha, Mhe. Naibu Waziri ametumia nafasi hiyo kuwapongeza Posta na AzamPesa kwa ubunifu huu utakaogusa maeneo mengi kiuchumi na kijamii, kwani kila mwananchi atapata huduma za kifedha kiurahisi huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya Kisera, Kisheria na Kitaasisi ili kuhakikisha huduma zinazowezeshwa na TEHAMA kama za kifedha kuleta tija kwa Taifa.
 

Kwa upande wake Postamasta Mkuu Bw. Maharage Chande ameeleza kuwa Ushirikiano huu ni moja ya mikakati ya Shirika unaojumuisha vikapu sita vilivyopo kwenye Mpango Mikakati mpya wa Shirika hususani kikapu cha Ukuaji wa Biashara. 

Vikapu hivyo ni pamoja na Watu, Wateja, Utendaji wenye ubora, Ukuaji wa Biashara, Teknolojia ya Ubunifu, na Masoko, huku akiahidi kutoa huduma bora kulingana na mahitaji ya wananchi.


 
Naye Mkurugenzi wa Mahusiano wa Makampuni ya Bakhresa Bw. Hussein Sufiani ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Sekta binafsi katika kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma mpaka mahali walipo.

Huduma hii ya AzamPesa ni huduma inayowezesha Wananchi kutuma na kupokea fedha pasipo makato yoyote  huku Shirika la Posta likiwa Wakala Mkuu (Aggregator) atakayetoa huduma hii ya AzamPesa katika ofisi zake zaidi ya 300 nchini Tanzania.

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA