JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

POSTA KUINGIA KAMATI YA MAAFA


POSTA KUINGIA KATIKA KAMATI YA KITAIFA YA MAAFA.

 

Shirika la Posta Tanzania leo limefunga rasmi mafunzo ya kukabiliana na maafa huku likitakiwa kuingia katika Kamati Elekezi pamoja na Kamati ya Wataalamu wa Maafa ziliyoko ndani ya Kamati ya Kitaifa ya Maafa iliyoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Consolatha Mbaga ambaye pamoja na mambo mengine alieleza majukumu ya kamati mbalimbali za maafa kuanzia ngazi ya taifa, mikoa, wilaya, tarafa hadi vijiji, ambapo Shirika la Posta linahusika moja kwa moja katika shughuli za maafa nchini kwani Shirika hilo linahudumia jamii pana ya wananchi kila siku kuanzia ngazi ya taifa hadi vijiji.

Katika upande mwingine, Shirika la Posta lilipata mafunzo ya huduma ya kwanza na uokoaji, yaliyotolewa na Mkufunzi wa Maafa kutoka Timu ya Wataalamu wa Ukoaji kutoka Mkoa wa Dar es Salaam "The Dar es Salaam Multi-Agency Emergency Response Team" (DarMAERT) Bw. Amini Mshana ambapo alionesha kwa vitendo namna ya kutoa huduma ya kwanza na uokoaji kwa waathirika wa majanga mbalimbali ikiwemo mafuriko, moto, anguko la majengo, ajali na magonjwa mbalimbali. 

Wafanyakazi hao wa Shirika la Posta walifanya kwa vitendo namna watakavyoweza kutoa huduma ya kwanza na uokozi ndani ya Shirika pamoja na mazingira yao ya kila siku.

Mafunzo haya ya kukabiliana na Maafa yaliyoratibiwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU), Ofisi ya Waziri Mkuu, na Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika la Posta yalianza tarehe rasmi tarehe 28 Novemba 2023 Jijini Dodoma, ambapo baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Posta kutoka Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika, Kitengo cha Udhibiti wa Vihatarishi na Ubora pamoja na wawakilishi wa baadhi ya Mikoa pamoja na Zanzibar.

Mafunzo hayo yametolewa ili kuwajengea uwezo na ujuzi watendaji na viongozi wa Shirika laPosta, ili waweze kuwa na uelewa wa Sheria ya Maafa 2015 na kanuni zake za mwaka 2017, waweze kujiandaa na kukabiliana na Maafa, kufanya tathmini ya Mahitaji Baada ya Maafa (PDNA) ndani ya Shirika, kuratibu na kufuatilia, usimamizi na tathmini ya ndani ya kukabiliana na Maafa pamoja na utoaji wa huduma ya kwanza na uokozi wakati wa maafa.

 

Imetolewa na;

Ofisi ya Mawasiliano, 

Shirika la Posta Tanzania. 

 

 

 

Mkufunzi wa Maafa kutoka Timu ya Wataalamu wa Ukoaji kutoka Mkoa wa Dar es Salaam (DarMAERT) Bw. Amini Mshana akionesha kwa vitendo namna ya kutoa huduma ya kwanza na uokoaji kwa waathirika wa maafa mbalimbali. 

Mkufunzi wa Maafa kutoka Timu ya Wataalamu wa Ukoaji kutoka Mkoa wa Dar es Salaam "The Dar es Salaam Multi-Agency Emergency Response Team" (DarMAERT)Bw. Amini Mshana akizungumza wakati wa mafunzo ya ya kutoa huduma ya kwanza na uokoaji kwa waathirika wa maafa mbalimbali.

Mkufunzi Mshauri Elekezi (Consultant) kutoka Umoja wa Posta Duniani, Bi. Vivaoliva Shoo akizungumza wakati wa mafunzo hayo.

Baadhi ya Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wakifanya kwa vitendo namna ya kutoa huduma ya kwanza na uokoaji kwa waathirika wa maafa mbalimbali. 

Baadhi ya Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wakifanya kwa vitendo namna ya kutoa huduma ya kwanza na uokoaji kwa waathirika wa maafa mbalimbali. 

Mratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Consolatha Mbaga akieleza majukumu ya kamati mbalimbali za maafa kuanzia ngazi ya taifa, mikoa, wilaya, tarafa hadi vijiji.

 

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA