JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

TPC LAFANYA MKUTANO WA WANAHISA


Shirika la Posta Tanzania limefanya Mkutano Mkuu wa Pili wa Mwaka wa Wanahisa leo, tarehe 11 Mei 2026, Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huu wa kihistoria ulizingatia taarifa ya utendaji kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambayo imeonesha mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na Shirika kupata Hati Safi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), na kugeuka kutoka kwenye kutengeneza hasara hadi kutengeneza faida.

Mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Balozi Meja Jenerali (Mstaafu) Gaudence Salim Milanzi, huku ukiwa umeandaliwa kwa lengo la kupitia kwa kina taarifa ya utendaji wa Shirika, kufanya maamuzi ya kimkakati ya kiuchumi, na kuweka msingi imara wa mustakabali wa Shirika katika kipindi cha Mpango wa Kibiashara wa Tisa (2026–2030).

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwanahisa Mkuu wa Shirika la Posta Bw. Nehemiah Kyando Mchechu, Msajili wa Hazina, Pamoja na wasaidizi wake ambao wameshiriki kwa njia ya mtandao.

Pia alishiriki Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Nikusubila Mwambije, pamoja na Bw. Paul Kwitega, Meneja Uhusiano wa Posta kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya Mkutano huo, Balozi Meja Jenerali (Mst.) Milanzi, alieleza mafanikio makubwa mawili ambayo Shirika lilifanikisha katika mwaka wa fedha 2024/2025:

Mosi, kupata Hati Safi (Unqualified Audit Opinion) kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ishara ya wazi ya uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali za umma.

Pili, Kutengeneza faida kwa mara ya kwanza baada ya kuwa na hasara katika mwaka wa fedha uliotangulia wa 2023/2024 mafanikio yanayothibitisha ufanisi wa mabadiliko ya kimkakati yaliyotekelezwa na Menejimenti.

“Kutokana na taarifa ya Utendaji kwa kipindi cha 2024/2025, Shirika limepata Hati Safi kupitia ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, na pia limetengeneza faida ikilinganishwa na hasara kwa kipindi cha mwaka uliopita. Hatua hii inadhihirisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma.” Amesisitiza Balozi Meja Jenerali (Mstaafu) Milanzi.

Naye, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Kyando Mchechu, alionyesha kuridhika kwake kwa mabadiliko na mageuzi ambayo Shirika la Posta Tanzania limeyafanikisha ndani ya kipindi kifupi. Alipongeza jitihada za Bodi na Menejimenti, na aliahidi ushirikiano endelevu wa Serikali katika kuliwezesha Shirika kufikia malengo yake ya kimkakati.

“Nimeona mwanga wa matumaini katika mageuzi makubwa yaliyofanywa na Shirika kwa kipindi kifupi sana. Niko tayari kuisaidia Bodi na Menejimenti kufikia malengo waliyojiwekea.” alieleza Bw. Mchechu.

Kwa upande wake, Bw. Paul Kwitega, Meneja Uhusiano wa Posta kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, alithibitisha mafanikio hayo na kusema hatua iliyofikiwa imewezesha uamuzi wa Mkutano wa Wanahisa kuridhia sehemu ya faida kutolewa kama gawio kwa Serikali, jambo linalothibitisha kuimarika kwa Shirika.

Naye mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Nikusubila Mwambije, alipongeza kwa dhati mafanikio ya Shirika na kusema Wizara imefarijika sana na mwelekeo chanya unaoonekana.

“Wizara inapongeza kwa dhati mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Shirika la Posta Tanzania. Mpito kutoka kwenye kutengeneza hasara hadi kutengeneza faida ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya mabadiliko na uongozi imara.” Mhandisi Nikusubila.

Pamoja na mafanikio ya sasa, Shirika la Posta Tanzania linajitayarisha kuanza utekelezaji wa Mpango wake wa Kibiashara wa Tisa, ambao utaanza mwezi Julai 2026 - 2030. Mpango huu unalenga kuimarisha ushindani, kuongeza ufanisi wa kiutendaji, kupanua huduma za kidijitali, na kuboresha huduma kwa wananchi wa Tanzania.
Miongoni mwa nguzo kuu za mpango huu ni pamoja na uimarishaji wa mifumo ya kidijitali, uanzishaji wa Jukwaa la Kitaifa la Biashara ya Mtandaoni, upanuzi wa huduma za kifedha wa vituo vya usafirishaji na utekelezaji wa miradi ya ubia nchini kote.

Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mwasiliano
Shirikala Posta Tanzania


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA