JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

TEKNOLOJIA KUFUATILIA MIZIGO NA MAPATO


 Yaingia makubaliano na Chuo cha Sayansi na Teknolojia Nelson Mandela ili kuwapa fursa wanafunzi kubuni teknolojia mpya

 Wakubaliana kuandaa mashindano ya kubuni teknolojia kuwavutia wanafunzi

 Posta sasa kutumia vifungashio vyenye teknolojia ya kisasa

Shirika la Posta Tanzania yazindua teknolojia yake mpya ya kufuatilia mizigo sambamba na teknolojia ya kufuatilia mapato yanayopatikana pindi mteja au kampuni inapofanya malipo huku lengo hasa likiwa ni kuboresha usalama wa mizigo ya wateja pamoja na kudhibiti mapato ya Shirika.

Hayo yamebainishwa na Postamasta Mkuu Bw. Maharage Chande tarehe 13 Juni, 2024 mara baada ya ufunguzi wa Jukwaa la Umoja wa Posta Duniani (UPU) katika jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) jijini Arusha. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Bw. Maharage ameeleza kuwa teknolojia hizo zitafungwa hadi kwenye vifungashio vya mizigo ili kudhibiti usalama wa mizigo mpaka pale itakapomfikia mteja.

Aidha, Maharage ameongeza kuwa, makubaliano waliyoingia na Chuo cha Sayansi na Teknolojia Nelson Mandela cha Arusha yana lengo la kuwapa fursa wanafunzi kushiriki katika kubuni Teknolojia mbalimbali za Posta, sambamba na kutumia Chuo hicho kuwaelimisha wanafunzi hao kuhusu huduma za Posta.

Naye kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Cha Sayansi na Teknolojia, Professa Maulilio Kipanyula amesema kuwa, ile dhana ya teknolojia ni fursa kwa uchumi jambo hilo limedhihirika kupitia makubaliano waliyoingia na Posta kwani wanafunzi wataweza kubuni teknolojia hizo na kupata kipato kupitia Posta

Profesa Maulilio ameongeza kuwa, kwa sasa wameungana katika safari ya mgeuzi ya kiteknolojia lengo ikiwa ni kuhakikisha teknolojia za Posta zinazobuniwa zinakamilika.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano

Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA